MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Yanga wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga, shukrani kwa bao la jiooooooni la mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube.
Dube alifunga bao hilo pekee dakika ya 87 ya mtifuano huo uliochukua nafasi kwenye dimba la Jamhuri jijini Dodoma, akiunganisha kimiani kwa kichwa pasi elekezi ya Mkenya, Duke Ogah Abuya, aliyepokea mpira wa Pacome Zouzoua.
Ni ushindi mwingine kwa Mreno Pedro Goncalves, aliyeinasa ajira ya kuwanoa Wana Jangwani hao baada ya kutimuliwa kwa mtangulizi wake Romain Folz.
Yanga imepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na alama 16 baada ya kushuka dimbani mara sita, pointi moja tu nyuma ya vinara JKT Tanzania waliojikusanyia alama 17 katika mechi 10 walizocheza.
Ushindi wa Yanga waliocheza bila Djigui Diara, Ibrahim Bacca na Clement Mzize, umekuja muda mfupi baada ya Watano wao Simba SC kuchapwa bao 2-0 katika Mzizima Derby dhidi ya Azam FC ya kocha Florent Ibenge.






No comments:
Post a Comment