Na Jackline Minja, MJJWM Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka kipaumbele katika ajenda ya ustawi na mifumo ya ulinzi wa mtoto, kuendeleza huduma za malezi mbadala, usimamizi wa Makao ya Watoto nchini ili kuhakikisha yanatoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa ziara ya kutembelea Makao ya Watoto ya Taifa Kikombo Jijini Dodoma na kujionea huduma zinazotolewa katika Makao hayo.

Mhe. Maryprisca amesema Makao ya Taifa ya Kikombo ni mfano wa Taasisi ya Serikali inayotekeleza majukumu hayo kwa weledi, upendo na dhamira ya dhati.
“Nimetembelea miradi, miundombinu na kupokea taarifa ya mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuimarishwa, nafurahishwa kuona jitihada kubwa zinazofanywa katika kutoa huduma ya Elimu, Afya, Lishe, ushauri nasaha pamoja na malezi kwa Watoto napenda kuwahakikishia kuwa Wizara itahakikisha Makao haya yanawezeshwa ipasavyo”. amesema Mhe. Maryprisca.
Aidha Mhe. Maryprisca ametoa rai kwa wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kuendelea kushirikiana na Wizara kwa kuwapa watoto fursa sawa za maendeleo kama ilivyo kwa watoto wengine wote wa Tanzania.
“Niwaombe Mashirika, wadau wa maendeleo tuendelee kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza makazi ya watoto ili wawe na huduma nzuri na wasijione wanyonge na niwaambie kuwa ninyi ni watu muhimu, mnapendwa na Taifa linawahitaji, msipoteze matumaini, someni kwa bidii, zingatieni maadili, muwe na nidhamu na mtumie fursa mnazopata ili mkafikie ndoto zenu."
amesema Mhe Maryprisca
Katika hatua nyingine Mhe. Maryprisca ameupongeza Uongozi wa Makao ya Taifa ya Kikombo kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha kuwa kila mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye upendo na yenye kumjenga.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema watumishi wa Makao hayo wana weledi na uwezo mkubwa wa kutambua uwezo wa watoto licha ya changamoto wanazokuja nazo watoto katika makazi hayo.
“Hawa watumishi unaowona hapa wanauwezo wa kukaa nao, kuongea nao kwa mbinu tofauti ndio maana nasema hawa sio watu wakawaida hata mimi wakiniangalia wanasema hapo hauko sawa, lakini ni miongoni mwa watu walioaminiwa na Serikali ambao watatusaidia kukiendeleza Makao haya”. amesema Wakili Mpanju.

Awali akisoma taarifa ya huduma zinazotolewa katika makao ya Taifa ya watoto kikombo Afisa Ustawi wa Jamii Anord Fyataga amesema hadi sasa kituo kimepata mafanikio mengi ikiwemo kuimarika kwa huduma za ushauri na unasihi ambapo kila mtoto anapata ushauri wa moja kwa moja au wa makundi, kuunganisha watoto 20 na familia zao, kuboreshwa kwa huduma za elimu ndani na nje ya makao ambapo wastani wa ufaulu wa watoto kwa shule za msingi na sekondari umeongezeka kwa asilimia mbili (2%) pamoja na kuwajengea ujuzi watoto 40 katika ujifunzaji wa stadi mbalimbali za maisha makaoni kama ushonaji wa nguo kwa kutumia cherehani.



No comments:
Post a Comment