Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewaasa wahitimu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kujiepusha na matendo maovu na elimu na maarifa waliyopata yawe tunu na faida kwa Taifa.
Mhe. Dkt Akwilapo ametoa wito huo tarehe 12 Desemba 2025 wakati wa mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) yaliyofanyika mkoani Morogoro ambapo jumla ya wahitimu 450 wa fani za Jiomatikia (Upimaji Ardhi), Upangaji Miji na Vijiji na Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) walitunukiwa Astashada na Stashahada katika fani hizo.
Mhe. Dkt Akwilapo amewataka wahitimu hao kukumbuka kuwa utii, nidhamu na tabia njema ni silaha itakayowafanya wapendwe mahali popote.
‘’Tukiwa hapa Morogoro tunakumbuka maneno yaliyoimbwa na mwanamuziki wa hapa hayati Mbaraka Mwinshehe na bendi yake ya Okestra Volcano; alisema “Heshima Kijana tanguliza kwanza mbele, ujeuri mbaya; uzuri si hoja tabia njema ni silaha utapendwa popote” mwisho wa kunukuu, alisema Mhe. Dkt Akwilapo.
Amewataka vijana kutodanganyika na maneno ya eti kuna watu wanaitwa Gen Z ambapo alieleza kuwa, hizo ni propaganda za kujenga hofu na kufifisha juhudi za nchi maskini kujitafutia maendeleo.
“Msidanganywe kuwa eti nyie ni kizazi cha vijana wasio na nidhamu, wapenda fujo, wasiosikiliza wazee wao, viongozi wao, chenye kujiamulia mambo yao bila kufuata sheria, taratibu, miongozo na tamaduni zetu; na mambo mengine ya hovyo’’ amesisitiza Mhe. Dkt Akwilapo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inasikitisha na kushangaza kuona vijana wa Kitanzania wanasikiliza maelekezo ya watu ambao hawaishi Tanzania na wala hawajawahi kuwaona na kupuuza maelekezo ya Viongozi wao na hata wazazi wao ambao wamewalea mpaka hapo walipoifikia.
Amesema, kuhitimu masomo kunatakiwa kuendane na uzalendo waliojengewa wa kuipenda Tanzania na kusisitiza kuwa waithamini nchi yao.
Mhe. Dkt Akwilapo amewataka kutumia utaalamu walioupata kwa weledi, uadilifu na kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo na kuepuka vitendo vinavyoenda kuhatarisha amani.
Vile vile amewataka kuendelea kujifunza kwani elimu ni bahari, haina mwisho na kuwataka wanaobaki chuoni kuongeza bidii katika masomo, nidhamu na kutunza amani na umoja kwani kesho yao inajengwa na maamuzi ya leo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bw. Musa Ramadhani Kilakala akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima amesema, migogoro ya ardhi imepungua mkoani humo hasa pale wizara ya ardhi ilipoanzisha Kliniki za Ardhi ambazo amezieleza zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao.
Akitoa taarifa kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda amesema chuo hicho kina Mpango Kabambe wa Miaka 20 (2023-2043) unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia na utendaji wa chuo katika kuwaandaa wataalamu wa sekta ya ardhi.
“Mpango kabambe huu unalenga kuongeza udahili wa wana chuo kutoka 660 hadi 5000, kuongeza watumishi kutoka 58 hadi 310 kuongeza program za mafunzo ya wanafunzi kutoka 2 hadi 7 pamoja na kujenga kampasi mpya katika eneo Mlima Kola mkoani Morogoro’’. Amesema Bw. Saguda.
.jpg)




No comments:
Post a Comment