Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kulinda walaji na kuimarisha viwanda vya ndani kwa kukamata na kuondoa sokoni zaidi ya mabati 700,000 yasiyokidhi viwango vya ubora.
Hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia viwango, kulinda haki za walaji na kukuza uchumi wa viwanda. Kwa kuimarisha ushindani wa haki na kuweka mazingira bora ya biashara, taifa linaweka msingi imara wa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wake.
Asubuhi na mapema katika maeneo yanayozunguka Kiwanda cha Mabati cha Lodhia kilichopo Kivule, mkoani Pwani , vikundi vya vijana hukusanyika wakisubiri kuanza zamu zao za kazi. Wapo wanaoshusha mizigo, wengine hupanga bidhaa ghalani, huku mama lishe wakianza kuwasha majiko yao tayari kuwahudumia wateja.
Kwa Rose Shirima, mama lishe anayefanya biashara jirani na kiwanda hicho, uwepo wa kiwanda umekuwa baraka kubwa. Ndani ya kipindi cha miaka miwili, kipato chake kimeongezeka kutoka shilingi 200,000 hadi kufikia shilingi Mil. 1 kwa mwezi.
"Awali nilikuwa napika chakula kidogo sana, lakini sasa nahudumia wafanyakazi wengi na hata wateja kutoka maeneo ya jirani,” anasema Rose kwa furaha.
Simulizi kama ya Rose inaonesha namna uwekezaji katika sekta ya viwanda unavyogusa maisha ya wananchi wa kawaida — kuanzia vijana wanaopata ajira hadi wanawake wanaoongeza kipato kupitia biashara ndogo ndogo.
Ni katika muktadha huo ndipo Serikali, kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ilipochukua hatua ya kufanya msako maalum na kukamata mabati yasiyokidhi viwango vya ubora, kufuatia maagizo ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba.
Maagizo hayo yalitolewa wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Mabati cha Lodhia, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa nchini zinazingatia viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
Tunaendelea na msako wa kidijitali ili kubaini na kuondoa bidhaa zisizokidhi viwango. Ni lazima bidhaa hizo ziondolewe sokoni kupisha wazalishaji wanaofuata taratibu na kanuni za uzalishaji wa bidhaa bora,” amesisitiza Waziri Kapinga.
Aidha, ameeleza kuwa hakuna mpango wa kutoa msamaha wa kodi kwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje ambazo tayari zinazalishwa hapa nchini. Uamuzi huo unalenga kulinda viwanda vya ndani, ajira za Watanzania na kuhimiza uzalishaji wa ndani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Lodhia, Arun Lodhia, amesema mafanikio ya kiwanda hicho yametokana na kuzingatia misingi ya utu, usalama kazini na ustawi wa wafanyakazi.
Amefafanua kuwa kampuni hiyo imeweka mazingira bora kwa wafanyakazi na jamii inayowazunguka, ikiwemo kuwasaidia mama lishe kwa kuwapatia majiko ya gesi, friji na huduma ya umeme bila malipo ili kuboresha biashara zao.
Naye Diwani wa Kata ya Kivule, Hassan Mahundu, amesema anajivunia uwepo wa viwanda katika kata hiyo, akibainisha kuwa vimechochea maendeleo na kukuza kipato cha wananchi wa eneo hilo.
Ni wazi kuwa safari ya kuelekea uchumi wa viwanda inahitaji nidhamu, uwajibikaji na usimamizi makini wa viwango.
Kupitia hatua hizi, Tanzania inaendelea kujenga taswira ya taifa linalothamini ubora, haki ya mlaji na ustawi wa jamii kwa ujumla — huku wananchi wanaozunguka maeneo ya viwanda wakishuhudia moja kwa moja matokeo ya sera hizo kupitia ajira, ongezeko la kipato na ustawi wa maisha yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa Bodi Kiwanda cha Lodhia Arun Lodhia.








No comments:
Post a Comment