HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

March 06, 2026

Waziri Prof. Mkenda Azindua Bodi Mpya ya TCU, Asisitiza Uimarishaji wa Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu ya Juu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), amezindua rasmi Bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), akiwataka Makamishna kuimarisha ubora wa elimu ya chuo kikuu nchini.


Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo Machi 6, 2026 Jijini Dar es Salaam na kuashiria mwanzo wa muhula mpya wa uongozi wa Bodi hiyo ambayo Mwenyekiti ni Prof. Makenya Maboko. 


Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bodi, Prof. Mkenda amesisitiza nafasi ya kimkakati ya TCU katika kusimamia, kuratibu na kuthibiti ubora wa elimu ya chuo kikuu kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Taifa. “Tume imebeba jukumu kubwa la kulinda ubora wa elimu ya juu pamoja na imani ya umma katika vyuo vikuu, vyetu” amesema Prof. Mkenda.


Halikadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa vyuo vikuu vinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia mifumo ya utawala bora sambamba na taratibu za uthibiti wa ubora wa elimu ili kupata wahitimu wenye elimu, maarifa, ujuzi na uwezo wa kustahimili ushindani kitaifa, kikanda na kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Tume, Prof. Maboko ameishukuru Serikali kwa imani iliyoiweka kwa Tume hiyo. Amesema kuwa Bodi itashirikiana kwa karibu na Sekretarieti ya Tume katika kuimarisha mifumo ya ndani ya uthibiti wa ubora wa elimu ya chuo kikuu pamoja na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyuo vikuu ili kuimarisha ukuaji na maendeleo endelevu ya elimu ya chuo kikuu nchini.

 

“Jukumu letu si la kiutawala pekee,” amebainisha Prof. Maboko. “Ni wajibu wa kimkakati kuhakikisha elimu ya chuo kikuu nchini inabaki kuwa yenye kuaminika, yenye ushindani na inayokidhi mahitaji ya soko la kitaifa, kikanda na kimataifa.” 


Hafla ya uzinduzi huo, ilitanguliwa na warsha ya Makamishna wa TCU iliyofanyika tarehe 5 hadi 6 Machi 2026. Warsha hiyo ya kimkakati ilijikita katika kutathmini hali ya elimu ya chuo kikuu nchini kwa kulinganisha mfumo wa elimu ya juu wa Tanzania na mifumo ya elimu ya juu katika nchi za Afrika ikiwemo Mauritius, Afrika Kusini na Kenya.

No comments:

Post a Comment

Pages