Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema mafanikio ya benki hiyo hayajengwi na ubora wa huduma, majengo au ufanisi pekee, bali yanatokana zaidi na imani ambayo wateja wameendelea kuipa benki hiyo.
Dkt. Nsekela alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja si tukio linalopaswa kuadhimishwa kwa kipindi cha wiki moja pekee, bali ni ukumbusho kwamba huduma bora kwa wateja inapaswa kutolewa kila siku.
“Huduma kwa wateja ni kila siku, si tukio la wiki. Lengo kubwa la wiki hii ni kujipima, kujitafakari na kuweka upya ahadi yetu kama taasisi na wadau ambao tumeaminiwa kutoa huduma kwa wateja wetu,” alisema.
Alisema maadhimisho hayo pia yanatoa fursa kwa CRDB kutathmini huduma zake na kujiuliza kama inatoa huduma zinazostahili kwa wateja wake.
“Ni kupima huduma zetu, kujipima sisi wenyewe kama tunastahili kusema kwamba kweli tumetoa huduma zinazostahili,” alisema.
Dkt. Nsekela aliongeza kuwa CRDB imeendelea kuboresha huduma za kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, huku ikiendelea kuthamini huduma zinazohusisha mawasiliano ya moja kwa moja na wateja.
Alisema pamoja na maendeleo ya teknolojia, bado kuna umuhimu wa kuwa na ‘human touch’, ili kuhakikisha wateja wanapata huduma yenye ukaribu, uelewa na kujali mahitaji yao. “Tumeboresha huduma za kidijitali, lakini bado tuna huduma za kukutana na watu ‘human touch’,” alisema.













No comments:
Post a Comment