NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amewashauri watumishi wa Manispaa ya Temeke kuwekeza katika hisa za Benki ya CRDB, akisema hatua hiyo inaweza kuwa na manufaa kwao katika kujiandaa na maisha ya baadaye.
Mapunda alitoa ushauri huo wakati wa hafla ya kupokea msaada wa meza na viti kutoka Benki ya CRDB kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kilungule, iliyopo katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
Alisema watumishi wanapaswa kuanza kufikiria namna ya kujenga vyanzo vingine vya kipato nje ya mishahara, ili kuwa na uhakika wa maisha yao ya baadaye.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Pwani wa Benki ya CRDB, Badru Idd, alisema benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida inayopata kila mwaka kwa ajili ya kurudisha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii.

Alisema fedha hizo hupelekwa katika maeneo makuu matatu ambayo ni elimu, afya na kukabiliana na majanga.
Kwa upande wa elimu, Idd alisema CRDB imekuwa ikisaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule, ujenzi wa madarasa, pamoja na utoaji wa vitabu, meza, viti na vifaa vingine vinavyohusiana na elimu.
“Faida ya benki tunayoipata kila mwaka huwa tunachukua asilimia moja tunaipeleka kwenye maeneo makuu matatu kama shukrani ya kusema asante kwa kufanya kazi na sisi,” alisema Idd.
Alisema eneo la pili ni afya, ambapo benki hutoa vifaa vya matibabu, kusaidia ujenzi wa vituo vya afya na hospitali, pamoja na mahitaji mengine yanayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, alisema sehemu ya faida hiyo hutumika kusaidia jamii wakati wa majanga mbalimbali, ikiwamo mafuriko yanayotokana na mvua kubwa na matukio mengine yanayoweza kuathiri maisha na makazi ya wananchi.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya CRDB ya kuhakikisha mafanikio ya benki yanaendelea kuwa na manufaa kwa jamii inayozunguka na kushirikiana nayo.









No comments:
Post a Comment