HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 05, 2015

VPL KUENDELEA KESHO

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wenyeji timu ya Azam FC watawakaribisha Mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu timu ya Young Africans.

Mechi hiyo no. 141 itachezeshwa na mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika vibendera Frednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (Dsm), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hussein Kalindo (Dsm) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian Mabena kutoka Tanga.

Katika mchezo huo timu ya Young Africans itakabidhiwa Kombe lake la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr Fennela Mkangara.

Mchezo huo wa kesho unatarajiwa kuanza majira ya saa 11 kamili jioni, kwa saa za Afrika Mashariki na kati ili kutoa fursa kwa wadau, wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kushudia mchezo huo pamoja na shamrashamra za kukabidhiwa kikombe.

Young Africans watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na mgeni rasmi, huku wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wakimkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili Mrisho Ngasa na fedha taslimu sh. millioni moja.


WAAMUZI WA KIKE TANZANIA KUCHEZESHA CONGO DR VS GABON
Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika - CAF limewateua waamuzi wa kike kutoka Tanzania kuchezesha mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake U-20 mwaka 2016 kati ya Congo DR dhidi ya Gabon.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa jumamosi tarehe 09.05.2015 jijini  Kinshasa - Condo DR, mwamuzi wa kati ni Jonesia Rukya, akisaidiwa na washika vibendera Dalila Jafari na Sophia Mtongoli huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hellen Mduma.

Wakati huo huo Elizabeth Kalinga ameteuliwa kuwa kamisaa wa mchezo kati ya Kenya dhidi ya Botswana kuwania kufuzu kwa michuani ya Olympiki, mchezo utakaofanyika Mei 31, 2015 nchini Kenya.


NB: Alhamisi ya tarehe 07 Mei, 2015, saa 5 kamili asubuhi, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) Mart Nooij ataongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages