HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 26, 2016

MUSWADA WA SHERIA ZA HABARI UTAIPA TASNIA HESHIMA

   Na Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es Salaam

WANATASNIA ya habari nchini wametakiwa kuukubali muswada wa sheria wa huduma ya habari unaotarajia kuwasilishwa hivi karibuni Bungeni kwa kuwa umekusudia kuifanya taaluma hiyo kuaminika kwa jamii.

Hayo yamasemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Hassan Abbas Jijini Dar es salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari vilivyopo Jijini humo.

Alisema kwa muda mrefu wadau wa Habari na wanatasnia wenyewe wamekuwa na kiu ya kupata sheria mpya baada ya ile ya mwaka 1976, ambayo imepitwa na wakati.

“Kutokana na teknolojia kubadilika, ni wakati mwafaka wa kuanzishwa kwa taasisi inayosimamia maadili ya wanahabari, hivyo vyombo vya Habari waliona ni muhimu kuwa na sheria mpya itakayokidhi mabadiliko hayo” alisema Abbas.

Aidha, alisema kuwa sheria hiyo itahusu vyombo vya habari vya mfumo wa machapisho, ambavyo ni pamoja na magazeti na majarida na si mitandao ya kijamii kama wadau wanatafsiri.

Aliongeza kuwa miongoni mwa masuala yanayozungumziwa katika muswada huo ni pamoja na kuundwa kwa bodi ya ithibati kwa wanahabari, Baraza huru la habari, Ofisi ya mkurugenzi wa habari, na Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.

Abbas aliongeza Serikali imewashirikisha wadau muhimu wakati wa mchakato wa kuandaa muswada huo ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha wamiliki wa vyombo vya habari (MOAT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na baadhi ya wadau wa haki za binadamu. 

Aidha alitoa wito kwa wadau wote kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha muswada huo sheria kupitia barua pepe ya ofisi ya Bunge can.bunge.go.tz ili kuyawasilisha mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Pages