HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 19, 2017

UJENZI WA BARABARA ZA KINDUNI, KICHUNGWANI, KITOPE ZITACHOCHEA MAENDELEO VIJIJINI

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akikagua jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kiombamvua lililojengwa na Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff kutekeleza ahadi za kusaidia huduma na Miradi ya Kijamii. Wa kwanza kulia ni Mshauri muelekezi wa Hoteli hiyo ya Sea Cliff ambae pia ni msimamizi wa Ujenzi wa jengo hilo la Skuli Nd. Yassir De Costa.
 Balozi Seif mbae pia ni Mwakilisihi wa Jimbo la Mahonda akikagua Bara bara ya Kinduni iliyopitia Kichungwani na kuelekea Kitope iliyojengwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar katika kiwango cha kifusi.
 Balozi Seif akizungumza na baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Kinduni na Kichungwani mara baada ya kuikagua bara bara iliyomo ndani ya Kijiji chao.
Mzee Juma Abdulrahman wa Kijiji cha Kichungwani  anayesumbuliwa na maradhi  ya macho na Miguu akitoa shukrani kwa niaba ya wanakijiji wenzake mbele ya Balozi Seif kwa hatuanjema iliyochukuliwa na Serikali kuijenga bara bara yao. Picha na – OMPR – ZNZ.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Ujenzi wa Barabara ya Kinduni, Kichungwani na hatimae kuelekea Kitope unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  utasaidia kuharakisha maendeleo ya Wananchi  hasa wakulima wa Vijiji hivyo.    

Alisema Ujenzi wa Bara bara hiyo ambao umo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM unatekelezwa  kufuatia ahadi iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mstaafu wa Awamu ya Sita Dr. Amani Karume.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Kinduni na Kichungwani baada ya kuikagua Bara bara hiyo iliyojengwa na Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar katika kiwango cha kifusi kuanzia Kinduni hadi Kichungwani.

Alisema Bara bara hiyo itakapokamilika rasmi itarahisisha mawasiliano ya usafiri kwa Wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao wanajishughulisha na kazi za Kilimo mchanganyiko katika kujipatia riziki zao za kila siku.

Balozi Seif  aliwahakikishia Wananchi hao kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hatua ya baadae ya Bara bara hiyo ni kuikamilisha katika kiwango cha lami ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.

Mapema Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum alisema  Bara bara ya Kinduni iliyopitia Kichungwani hadi Kitope ni miongoni mwa Bara bara za ndani lakini kwa agizo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein itajengwa katika kiwango cha Lami.

Mh. Mohamed alisema Ahadi zote  za Chama cha Mapinduzi zilizotolewa kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 zitaendelea kutekelezwa na Wizara yake kwa  upande wa Sekta ya Mawasiliano.

Alisema ahadi zozote zinazotolewa na Viongozi Wakuu popope pale ni agizo maalum linalostahiki Taasisi au watendaji wahusika kuzitekeleza kulingana na mazingira yaliyowazunguuka.

Naye Mzee Juma Abdulrahman akikaguliwa na Mh. Balozi Seif  kutokana na hali yake ya afya Kijijini hapo kwa niaba ya wananchi wenzake aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa Bra bara hiyo.
Mzee Juma alisema Bara bara hiyo iliyokuwa kilio cha miaka mingi kilicholeta changamoto na matatizo kwa Wananchi hao itakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa wakulima pamoja na kizazi kijacho.

Alisema kero la Bara  bara hiyo ilipelekea wananchi Vijiji hivyo wakati wa Awamu zilizopita walilazimika kukata miti ilimradi kupunguza usumbufu waliokuwa wakiupata hasa kwa akina Mama waja wazito wanapokwenda kujifungua.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitembelea Jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kiombamvua lililomaliza ujenzi wake.

Jengo hilo limejengwa na Uongozi wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff  ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake ilizotowa wakati wa Vikao vyake mbele ya Kamati ya Bandari ya Kiombamvua kwamba itasaidia huduma na miradi ya maendeleo ya Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/2/2017.

No comments:

Post a Comment

Pages