HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 21, 2017

DC DODOMA AWATAHADHARISHA WATAKAODANGANYA KATIKA ULIPAJI FIDIA ENEO LA UJENZI WA UWANJA WA MICHEZO NALA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Christina Mdeme akizungumza na wakazi wa Kata ya Nala alipowatembelea na kusikiliza maoni na changamoto mbalimbali zilizopo katika kuanza kutekelaza radi wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Kimataifa Dodoma. 
Diwani wa Kata ya Nala Mhe. Brayceon Leonard Eliah akiwasisitiza wakazi wa Kata yake kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kutekeleza mradi huu wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Kimataifa.   
 Afisa Mipango Miji Manispaa ya Dodoma Bw. Clemence Msuva akieleza taratibu za tathimini ya eneo lililopo katika Kata ya Nala utakapojengwa uwanja wa Michezo wa Kimataifa zitavyofanyika ili kuwezesha mradi huo kuanza mapema.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Nala wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Christina Mdeme(Hayupo Pichani) alipowatembelea na kusikiliza hoja mbalimbali juu ya mradi wa ujenzi wa wa Uwanja wa Michezo wa Kimataifa unaotarajiwa kujengwa Mjini Dodoma.


Na Raymond Mushumbusi, WHUSM Dodoma


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Christina Mdeme amewatahadharisha wakazi wa Kata ya Nala watakaofanya aina yoyote ya udanganyifu katika ulipaji fidia kwao kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Kimataifa utaojengwa Mjini Dodoma.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Nala alipowatembelea na kusikiliza hoja mbalimbali juu ya mradi wa ujenzi wa wa Uwanja wa Michezo wa Kimataifa unaotarajiwa kujengwa Mjini Dodoma.

“Wewe kama unajijua sio mkazi halali wa eneo unapopita mradi huu naomba ukafute jina lako ila tukikubaini tutakuchukulia hatua kali za kisheria” alisisitiza Mhe. Christina.

Mhe. Christina Mdeme ameongeza kuwa Serikali haipo tayari kupoteza hela kwa ajili ya kulipa watu wasiostahili katika mradi huo na kwamba  kila anayehusika kulipwa fidia kihalali atalipwa.

Aidha Mhe. Christina Mdeme amewahakikishia wakazi wa Kata ya Nala kuwa Serikali haitamdhulumu mtu yoyote na atahakikisha kila anayepaswa kulipwa fidia analipwa fidia anayostahili.

Pia amewatahadharisha wakazi hao kutotumiwa na viongozi au vikundi vya watu kwa manufaa ya kujipatia pesa zinazotokana na fidia za mradi huo kwa njia za udanganyifu.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Evordy Kyando amewaomba wakazi wa Kata ya Nala kuwa watulivu na kwamba Sheria na Taratibu za ulipaji fidia zitafuatwa kikamilifu katika zoezi hilo.

Akitoa maelezo ya kwa niaba ya Kamati ya Mkoa ya Uratibu Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Kimatafa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw.Salum Mkuya amewahikikishia wakazi wa Kata ya Nala ushirikiano kutoka kwa Kamati yake ili kufanikisha mradi huu wa kimataifa.

Akizungumza kabla ya kufunga mkutano huo Diwani wa Kata ya Nala Mhe. Brayceon Leonard Eliah amewaomba wakazi wa Kata yake kutoa ushirikiano kwa maafisa wa Serikali watakaokuwa wanatathimini maeneo yao kwa ajili ya ulipaji wa fidia.

No comments:

Post a Comment

Pages