HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 30, 2017

Madhara lishe duni ni zaidi ya athari za rushwa

•Wataalamu wataka hatua kukoa matrilioni ya fedha


NA HAPPINESS MNALE

MIONGONI mwa mambo ambayo serikali ya Awamu ya Tano imeyapa kipaumbele ni kuundwa kwa Mahakama ya Makosa ya Rushwa.

Tayari sheria za mahakama zimefanyiwa marekebisho na sasa Majaji 14 wako ‘darasani’ wakinolewa kwa ajili ya kuwezesha mahakama hiyo kuanza kazi yake, ikiwa imepita miezi minane tu, tangu Rais John Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015.


Msukumo wa kuanzishwa haraka kwa Mahakama hiyo, unatokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo vimeitikisa nchi kwa zaidi ya miaka 20 na kusababisha upotevu wa fedha nyingi.

Miaka kumi iliyopita chini ya utawala wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, tatizo la rushwa liliongezeka. Zilisikika kashfa kadhaa za rushwa, ukiwamo wizi wa Sh.133 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kashfa Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo pia ilikuwa BoT ikihusisha zaidi ya Sh. 300 bilioni.

Ripoti iliyotolewa Desemba 2014 na taasisi ya kimataifa iitwayo Global Financial Intergrity (GFI) inaonyesha kuwa Tanzania imekuwa ikipoteza karibu Sh.trilioni moja kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 3.4 ya bajeti ya serikali kwa huu wa fedha kinachofikia sh.trilioni 29.5.

Inawezekana mazingira hayo ndiyo yaliyoweka msukumo wa kuharakishwa kwa mchakato wa kuanzishwa kwa Mahakama, lengo likiwa ni kuokoa fedha za nchi zinazopotelea mikononi mwa wajanja wachache.

Mazingira yaliyoisukuma serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya vitendo vya rushwa, pia yanapaswa kuisukuma kulitupia jicho eneo la lishe katika jamii ya Watanzania ambayo kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu, ghamara yake kwa nchi ni kubwa kuliko madhara ya rushwa kifedha.
Matokeo ya Makadirio ya Kitaalamu yaliyofanywa na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2014, yakishusu athari za lishe duni, yanabainisha wazi kwamba ikiwa hali itabaki kama ilivyo sasa, Tanzania itapoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa miaka kumi ijayo.

Takwimu za sasa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kutokana na lishe duni, zadi ya watoto milioni 2.7 nchini wamedumaa, huku 446,000 kiwa na tatizo la ukondefu na 106,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Licha ya kwamba hali ya udumavu nchini kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano imepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34 miaka miwili iliyopita, kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa lishe na chakula nchini wa 2014, lakini hali bado ni mbaya katika baadhi ya maeneo nchini.

Utafiti wa kitaalamu

Timu iliyofanya makadirio ya kitaalamu kuhusu athari za lishe duni, ilitoa taarifa yenye sura mbili; kwanza ni makadirio ya nafuu ya kifedha itakayopatikana ikiwa hatua zitachukuliwa kukabiliana na athari za lishe duni na pili ni gharama kwa maana ya hasara ya kifedha ikiwa hali itabaki kama ilivyo sasa.

Chini ya ufadhili wa Shirika la Msaada la Marekani (USAID), kupitia Mpango wa Kusaidia Chakula la Lishe (FANTA), wataalamu hao wakijumuisha wale wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC), wanasema kati ya mwaka jana 2014 hadi 2025, Tanzania inaweza kuwa imepoteza zaidi ya sh.trilioni 32.6 ikiwa hali itabaki kama ilivyo.


Sh.trilioni 32.6 ni jumla ya fedha zinazotokana na matatizo katika maeneo matatu; udumavu ambao unaweza kusababisha gharama (hasara) ya sh.trilioni 28.8, magonjwa ya anaemia yanayotokana na upungufu wa madini chuma miogoni mwa mwa watu wazima na wanawake wasio wajawazito sh.trilioni 2.3 na ukosefu wa madini joto mwilini sh.trilioni 1.5.

Fedha hizo kwa ujumla wake ni zaidi ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/2017 ambayo ni sh.trilioni 29.5.

Kwa upande mwingine takwimu hizo zinamaanisha kuwa, gharama ya kuendelea kuwa na matatizo au magonjwa yatokanayo na lishe duni ni zaidi ya wastani wa sh.trilioni 3 kwa mwaka, kiasi ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha zinazopotea kutokana na vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Mtaalamu wa Bajeti wa TFNC, Samson Ndimanga anasema gharama ya kukabiliana na matatizo hayo ni ndogo ikilinganishwa na hasara inayokadiriwa kwa miaka kumi ijayo, hivyo uwekezaji katika eneo hilo unaweza kulipa taifa nafuu katika matumizi ya rasilimali zake.

Ndimanga alisema takwimu za tathmini zinaonyesha kuwa ikiwa hatua zitachukuliwa kukabiliana na matatizo yanayotokana na lishe duni, Tanzania inaweza kuokoa kiasi cha sh.trilioni 7.62 kwa miaka kumi na kukwepa hasara inayokadiriwa.

Fedha hizo ni sh.trilioni 6.237 kutokana na mafanikio ya vita dhidi ya udumavu, sh.bilioni 767 kutokanana kuyakabili vilvyo matatizo yatokanayo na ukosefu wa madini joto, wakati kwa magonjwa ya upungufu wa damu na madini chuma, zinazweza kuokolewa sh.bilioni 611.


Ndimanga anasema makadirio yaliyofanya yalizingatia ongezeko linaloweza kutokea kwa waathirika wa matatizo hayo, gharama za matibabu kwa maana ya muda, madaktari, vifaa tiba na dawa kwa ajili ya magonjwa yatokanayo na lishe duni.

Matatizo ya lishe Tanzania

Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii, Dk. Sabas Kimboka alisema serikali imeendelea kupoteza fedha nyingi kutibu magonjwa yatokanayo na lishe.

Dk. Kimboka alisema matatizo mengi ya utapiamlo nchini yanayotokana na upungufu wa virutubishi mwilini kutokana na watu kukosa nishati na protini, wekundu wa damu, upungufu wa vitamini A na wa madini ya joto.

“Hali hizo zinaweza kusababishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha na chenye virutubishi muhimu na magonjwa,”anasema Dk. Kimboka.

Anasema TFNC imekuwa ikitoa elimu kupitia maofisa lishe waliopo katika halmashauri zote nchini, ikiwa ni hatua ya kupunguza matatizo yatokanayo na lishe duni.

Anataja vyakula vilivyowekewa virutubishi hivyo ni unga wa ngano ambao unaongezwa virutubishi vya vitamin B12, asidi ya foliki, madini ya chuma na madini ya zinki,unga wa mahindi ambao unaongezwa virutubishi vya vitamin B12, asidi ya foliki, madini ya chuma na madini ya zinki, mafuta ya kula ambayo yanaongezwa vitamini A na vitamini E na chumvi ambayo inaongezwa madini joto.



Lishe inapatikana wapi?

Takwimu za kitafiti zilizotajwa ni ushahidi kwamba matatizo yatokanayo na lishe duni yameendelea kuiingiza nchi katika gharama ambazo kimsingi zinaweza kuepukwa.



Mtaalamu wa Lishe, watoto na wanawake katika Hospitali ya Sinza jijini Dar es Salaam, Dk. Itael Makele anasema lishe bora ni muhimu kwa binadamu na haijali umri wala rika la mtu.Kwa maelezo ya mtaalamu huyo wa tiba, virutubishi katika mwili ni matokeo ya mtu anavyoweza kuapata chakula bora na kwamba lishe ni sayansi ya namna mwili unavyokitumia chakula hicho.



Dk. Makele ansema lishe bora husaidia kutengeneza na/au kurudisha seli za mwili zilizokufa, kusaidia ukuaji wa akili na mwili, kuupa mwili nguvu, joto na uwezo wa kufanya kazi pamoja na kuuwezesha mwili kujikinga na maradhi mbalimbali.Anasema chakula mchanganyiko na cha kutosha, husaidia kumpatia binadamu mahitaji yake yote ya kilishe, ambayo ni kujenga, kulinda na kuupa mwili nguvu na kwamba vyakula vyote vina virutubishi zaidi ya kimoja na kila kirutubishi kina kazi yake katika mwili wa binadamu.



Dk. Makele anasema ili binadamu apate lishe bora anahitaji vyakula vyenye virutubishi vya aina tano, ambavyo ni kabohaidreti, vitamini, protini, madinijoto na madini chuma pamoja na maji.

Kabohadreti ni vyakula vya wanga, mafuta ya wanyama na mimea ambavyo kwa mujibu wa Dk. Makele husaidia kuupa mwili nguvu kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali pamoja na joto.
“Kabohaidreti ndio inayochukua sehemu kubwa ya mlo na hii hupatikana katika mahindi, mchele, uwele, ngano, viazi vya aina zote, mihogo, ndizi, magimbi na mtama,”alisema.



Dk. Makele anasema Protini husaidia mwili kutengeneza seli mpya, kutengeneza vimeng’enyo mbalimbali na wakati mwingine protini huupa mwili nishati, wakati mafuta husaidia usharabu wa baadhi ya vitamin na kulainisha chakula.Kuhusu maji Dk. Makele anasema ingawa hayahesabiwi kama kundi la chakula, lakini yana umuhimu mkubwa katika lishe ya binadamu.



“Inapaswa kunywa maji ya kutosha, angalau lita moja na nusu sawa na glasi nane kwa siku au hata zaidi, vilevile mtu anaweza kuongeza maji mwilini kwa kunywa vinywaji kama supu, madafu na juisi za matunda,”anasema.Kwa maelezo ya wataalamu wa afya na lishe, ni dhahiri kwamba matatizo ya lishe duni yanaweza kupata majawabu bila kutumia fedha nyingi kama inavyohitajika katika maeneo mengine kama ilivyo katika vita dhidi ya rushwa.Kwa kuwa kuzuia ni bora kuliko kuponya, uwekezaji pekee mkubwa ambao nchi inaweza kuufanya, ni kutoa elimu ya lishe kwa kwa jamii ya Watanzania, ili kila mmoja atambue kwamba lishe bora ni sawa na kutibu magonjwa kwa maelfu asiyoyaona.
mnaleh@hayoo.com

No comments:

Post a Comment

Pages