HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2017

WAJASIRI WAIOMBA SERIKALI KUWAJENGEA MAZINGIRA MAZURI YA ULIPAJI KODI

Na Mwandishi Wetu


WAJASIRIAMALI wameiomba Serikali kujenga mazingira ya ulipaji kodi na malipo anuai ya vibali vya biashara kufanyika eneo moja ili kupunguza urasimu ambao wamekuwa wakiupata wafanyabiashara wanapoitaji kulipia tozo hizo. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Plus Events Cards, Bi. Rehema Moses alipokuwa akizinduwa tawi jipya la uuzaji kadi jumla na rejareja kwa ajili ya matukio mbalimbali ya sherehe eneo la Mwenge, Sokoni jijini Dar es Salaam.

Bi. Moses alisema wapo wafanyabiashara waadilifu ambao wanajua umuhimu wa kulipia tozo mbalimbali na vibali vya biashara wanazozifanya lakini baadhi wamekuwa wakikwazwa na urasimu uliopo katika ufuatiliaji wa vibali hivyo na mtawanyiko wa ofisi anuai za kufanyia malipo, jambo ambalo linachangia kujikuta wanashindwa kulipia kwa wakati.

Mfanyabiashara huyo mwanamama na Mtanzania wa kwanza kusambaza bidhaa hizo za kisasa aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa vibali vyote na malipo kuwa yakifanyika eneo moja ili kumrahisishia mfanyabiashara kukamilisha vibali husika kwa wakati, na kumpunguzia mfanyabiashara vikwazo ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikimpotezea muda mwingi katika ufuatiliaji.

"...Kuna haja ya Serikali kupitia mamlaka husika kuangalia namna gani ya kupunguza urasimu wa ufanyaji malipo ya kodi na vibali mbalimbali vya biashara. Unajua mfanyabiashara ana muda mchache sana katika kushughulikia masuala yake hivyo anapozunguka muda mrefu kupoteza muda kufuatilia ama vibali au malipo ya tozo ofisi mbalimbali anapoteza muda bila ulazima...binafsi nazishauri mamlaka husika kuangalia namna ya kupunguza mizunguko hiyo na malipo yafanyike ofisi moja," alisema Bi. Rehema Moses.

Aidha alivishauri vyombo vya kudhibiti ubora wa bidhaa kuongeza nguvu ili kudhibiti baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakichapisha kadi feki nchini na kuwalaghai watanzania kuwa ni halisi, jamboa ambalo linawaharibia wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa halisi. Alisema kampuni yake ambayo imekuwa ikisambaza kadi za kisasa za matukio mbalimbali ya sherehe jumla na rejareja kutoka nchini China ipo tayari kuwasaidia wajasiliamali waaminifu kutoka popote nchini kufanya biashara hiyo bila udanganyifu ili kumpatia mlaji wa mwisho bidhaa halisi kwa bei nzuri.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa tawi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi. Doris Mollel akizungumza na wanahabari aliwashauri wananchi kupenda kununua bidhaa halisi na kuachana na bidhaa feki kwani zimekuwa na madhara huku zikilikoseshea taifa mapato. Alisema bidhaa nyingi feki haziingii kwa utaratibu rasmi nchini hivyo licha ya madhara kwa watumiaji zimekuwa zikilikosesha taifa mapato.

"...Nashauri Watanzania wenzangu tupende kununua bidhaa halisi zinazoendana na thamani ya fedha tunazotoa. Uzuri sasa hivi wauzaji wengine wamekuwa wawazi wanakwambia hii ni bei rahisi kwa kuwa ni feki na hii ndio bidhaa halisi...tujenge utamaduni wa kutumia bidhaa bora na halisi kwa manufaa yetu na taifa," alisisitiza Bi. Doris Mollel.

Mkurugenzi huyo aliipongeza kampuni ya Plus Events Cards kwa kusogeza huduma zake eneo la Mwenge na kutoa fursa kwa wajasiriamali kuwatembelea kwa ajili ya kusambaza bidhaa hizo Dar es Salaam na hata mikoani. Aliongeza kuwa hatua hiyo si tu imesogeza huduma kwa wahitaji bali imetoa fursa kwa wajasiriamali wadogo kupata bidhaa za kadi kirahisi na kuzisambaza kwa wahitaji.

No comments:

Post a Comment

Pages