HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 02, 2017

RAIS KARIA ASHINDA UJUMBE CECAFA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameshinda nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
 
Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Desemba 2, 2017 jijini Nairobi, Kenya Rais Karia alipita bila kupingwa kuwa Mjumbe CECAFA.
Awali kinyanganyiro hicho kiliwavutia wanachama wanane kabla ya watatu kujiondoa na hivyo watano hao kuchaguliwa bila kupingwa.

Wajumbe hao ambao wataungana na Rais wa CECAFA, Mhandisi Mutasim Gafar wa Sudan watakuwa na kibarua kuboresha utenda kazi wa baraza hilo kwa ajili ya kuimarisha soka ukanda huo.

Wengine waliochaguliwa ni Abdiqaani Arab Said (Somalia), Aimable Habimana (Burundi), Juneid Basha Tilmo (Ethiopia) na Mwanamke Petra Dorris wa Kenya.
 
KILIMANJARO STARS KIBARUANI KESHO
 
Kilimanjaro Stars - Timu ya Taifa ya Tanzania Bara kesho Jumapili Desemba 3, 2017 itacheza na Libya katika mchezo wa pili wa michuano ya kuwania Kombe la CECAFA - linaloandaliwa na Baraza la Soka la Afrika Mashariki.
 
Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Machakos, utaanza saa 10:00 jioni (1600h) mara baada ya mchezo wa kwanza kati ya Kenya ‘Harambee Stars’ na Amavubi ya Rwanda utakaoanza saa 8.00 alasiri (1400h) utakaofanyika Uwanja wa Kakamega.
 
Michezo hiyo kama ilivyo kwa michezo mingine katika michuano hiyo itakuwa mubashara kutoka Kenya kwenye vituo mbalimbali vya televisheni ikiwamo Azam TV ya Tanzania.
 
Kilimanjaro Stars tayari wana shime kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ammy Ninje.

“Msidharau mechi,” alisema Dk. Mwakyembe wakati wa hafla ya chakula cha jioni ambako alitumia baraza hilo kuwaaga vijana hao akiwataka wachezaji wa timu hiyo kwenda Kenya kujitahidi iliyofanyika Novemba 29, mwaka huu.

Wachezaji waliko Kenya ni makipa Ramadhani Kabwili (Young Africans, Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
 
Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
 
Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya), Ibrahim Ajib (Young Africans) na Amani Kiata wa Nakuru All Stars ya Kenya.

Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat), Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes) na Yahya Zayd kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.
 
Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu mwenye Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
……………………………………………………………………..……………..……

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages