HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 20, 2018

WAZIRI MKUU AMKABIDHI MKURUGENZI WA MUWASA KWA TAKUKURU

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Maji Musoma, Mhandisi Said Gantala (kushoto) akitoka kwenye ukumbi wa Balili Rock Resort  mjini Bunda baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuamuru kuwa akamatwe na ahojiwe na TAKUKURU Januari 19, 2018. Kulia ni Kamanda wa TAKUKURU  wa mkoa wa Mara, Alex Kuhanda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA) Mhandisi Gantala Said kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Bunda.

Mbali na Mkurugenzi huyo pia TAKUKURU inawashikilia wakandarasi wanaojenga mradi huo ambao ni Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang'anyi  Bw Mauza Mmangi ambaye ndiye mkandarasi anajenga mradi huo unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye eneo la Nyabehu hadi Bunda mjini.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na Mhasibu wa Kampuni ya Ujenzi ya Nyakirang'anyi Bw. Amon Gideon pamoja na viongozi wa kampuni nyingine ya ujenzi ya Fortrss Bw. Juvenari Chirianga na Ephraim Mpeko ambao nao walishiriki katika ujenzi wa mradi huo.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo jana jioni (Ijumaa, Januari 19, 2018) baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kueleza sababu zilizosababisha mradi wa maji Bunda kutokamilika  pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi.

Akizungumza katika kikao maalumu cha kujadili changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, alichokiitisha mjini Bunda, Waziri Mkuu alisema aliamua kuitisha kikao hicho baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo hususan inayosimamiwa na MUWASA.

Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo  inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji. 

Waziri Mkuu amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kupitiwa upya kwa mradi huo   kwa sababu hafurahishwi na ujenzi wake.” Kama Mkurugenzi wa MUWASA anasema mradi umekamilika kwa asilimia 98 sasa kwa nini wananchi walalamikie kukosa huduma hiyo.”

Alisema Mkurugenzi huyo amekuwa akimlipa mkandarasi fedha kabla ya kufanya kazi ambapo hadi sasa tayari mkandarasi anayejenga mradi huo ameshalipwa zaidi ya sh. bilioni saba na mradi haujakamilika na wananchi wanaendelea kutumia maji ambayo siyo salama.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wahojiwe na wakibainika kuhusika na ubadhilifuu wa fedha za mradi huo, wachukuliwe hatua kali za kisheria.”Serikali imedhamiria kuimarisha huduma za maji, hivyo hatuhitaji mtu atakayeenda kinyume na mpango huo.”

Mradi wa kupeleka maji kwenye mji wa Bunda maji kutoka ziwa Victoria katika eneo la Nyabeho ulisanifiwa mwaka 2006 na ulikuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Malima aliagiza kufungwa na ofisi za MUWASA na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, JANUARI 20, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages