HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 15, 2012

BLATTER, PLATIN KUIJADILI ADHABU YA SERBIA

Rais wa FIFA, Joseph 'Sep' Blatter

TOKYO, Japan

"Tutakaa na Uefa kuzungumzia aina sahihi ya adhabu zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa kama haya katika soka – na hii sio kwa Uefa tu, bali kwa mashirikisho yote ya soka ya mabara na vyama vya kitaifa. Lazima tuwe thabiti, wenye nguvu, tena wakali"

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter amesema anapanga kukaa mezani na Rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa), Michel Platini kujadili adhabu waliyopewa Chama cha Soka cha Serbia. 

FA ya Serbia imepigwa faini ya pauni 65,000 na Uefa, baada ya kukutwa na hatia ya udhalilishaji na ubaguzi wa rangi uliofanywa na mashabiki na wachezaji wa timu ya vijana, wakati wa mechi dhidi ya vijana wenzao wa U-21 wa England Oktoba mwaka huu.

"Nitakuwa na mkutano na Rais wa Uefa," alisema Blatter, alipoongea kwenye mkutano na vyombo vya habari jijini hapa na kuongeza: "Lakini sijui kama (Platini) ana ushawishi kwa Kamati ya Nidhamu ya Uefa kuweza kuyatazama upya maamuzi yao."

Platini ameripotiwa kutafakari rifaa kwa Kamati ya Nidhamu iliyo chini ya shirikisho lake juu ya ukali wa adhabu hiyo ambayo pia imefunga milango ya Serbia kushiriki michuano ijayo ya vijana wa U-21.

Wachambuzi wa masuala ya soka wameishangaa faini iliyopigwa Serbia, huku wakilinganisha na ile ya pauni 80,000 ya aliyolimwa Nicklas Bendtner kwa kuonesha tu nembo ya mdhamini wake wa nguo za ndani wakati wa fainali za Mataifa Ulaya 2012. 

Katika mkutano huo, Blatter alikwepa kujibu swali aliloulizwa na mwandishi wa BBC Sports kama haoni kuwa adhabu ya Uefa kwa Serbia ni rafiki mno kwa wabaguzi wa rangi na wadhalimu viwanjani.

Badala yake akajikuta akijibu: "Nina uhakika kwamba tutakaa na Uefa kuzungumzia aina sahihi ya adhabu zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa kama haya katika soka – na hii sio kwa Uefa tu, bali kwa mashirikisho yote ya soka ya mabara na vyama vya kitaifa.

"Lazima tuwe thabiti, wenye nguvu, tena wakali hasa linapokuja suala la ubaguzi wa aina yoyote, ukiwamo huu tupigao vita kila uchao wa rangi," alisisitiza Blatter

No comments:

Post a Comment

Pages