HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2013

BLACK LEOPARDS WATAMBA KUIFYATUA YANGA LEO


DAR ES SALAAM, Tanzania

“Hii ziara yetu ya kwanza Tanzania. Tumefanya hivi Zimbabwe na nchi nyingie na huko tulipata matokeo mazuri, tunayotarajia tutaendelea kuyapata tukiwa hapa Tanzania dhidi ya Yanga kesho”

KOCHA wa timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini, Abel Makhubela, ametamba kushinda pambano lao la leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Yanga, akijivunia uzoefu wa kikosi chake katika michuano ya kimataifa.

Makhubela aliyasema hayo jana alasiri baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere, akiwa miongoni mwa viongozi 11 na wachezaji 23 wa Black Leopards, waliosafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).

Kocha huyo aliongeza kusema kuwa, uzoefu walionao kutokana na ziara katika mataifa mbalimbali Afrika – kwa mechi za kirafiki na kimashindano, unampa matumaini ya kufanya vema dhidi ya Yanga, huku akikiri kuwa kuja Tanzania ni faraja kwa kikosi chake.

“Hii ziara yetu ya kwanza Tanzania. Tumefanya hivi Zimbabwe na nchi nyingie na huko tulipata matokeo mazuri, tunayotarajia tutaendelea kuyapata tukiwa hapa Tanzania dhidi ya Yanga kesho. Nimekuja na wachezaji wangu wote wa kikosa cha kwanza, jumla ya wachezaji ni 23, mashabiki watarajie mchezo mzuri,” alisema Makhubela.

Aliongeza kuwa, wanaijua Yanga kuwa ni timu nzuri kama ilivyo kwa mahasimu wao Simba – ambazo ni miongoni mwa timu maarufu barani Afrika, hivyo wamejiandaa vya kutosha, akiamini mechi hiyo itakuwa ni kipimo kizuri kwao, kwa ajili mechi zijazo za Ligi Kuu ya kwao (PSL) inakoshika nafasi ya 12.

Akizungumzia ujio wa Leopards, Mratibu wa mechi hiyo, Shaffih Dauda wa Prime Time Promotions, alisema jana kuwa maandalizi yote yamekamilika na kuwa wamepunguza kiingilio cha shilingi 5,000 na kuwa 3500, ili kuwafanya mashabiki wengi kuona mechi hiyo.

Viingilio vingine katika mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 alasiri, ni shilingi 7,000 kwa viti vya rangi ya machungwa, 15,000 kwa VIP C, 20,000 kwa VIP B na shilingi 30,000 kwa VIP A,

Dauda aliongeza kuwa, Black Leopards wamefikia katika Hoteli ya Seascape iliyoko Mbezi na wako tayari kwa mechi hiyo inayosikindikiza mkutano mkuu wa Yanga utakaofanyika kesho Jumapili kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, na kurushwa ‘live’ na Clouds Tv.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Wanajangwani hao, Baraka Kizuguto, alisema wana furaha kwa ujio wa Leopards, akimini itatoa changamoto tosha kwa kikosi chao na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi leo kuwapa sapoti vijana wao.

“Hii ni mechi ya kwanza mwaka huu katika ardhi ya nyumbani. Mashabiki wetu waje kwa wingi kuona matunda ya ziara yetu ya wiki mbili nchini Uturuki.

“Tulifanya mazoezi ya kutosha kule, tumefanya hivyo pia baada ya kuwasili na  sasa ni zamu ya mashabiki kuona tumevuna nini katika maandalizi yetu,” alisisitiza Kizuguto.

No comments:

Post a Comment

Pages