Na Elizabeth John
MUIGIZAJI wa filamu nchini, Mohamed Nurdin
‘Chekibudi’ amewashukuru wadau na wapenzi wa kazi zake baada ya kumpokea vizuri
na kazi yake inayokwenda kwa jina la ‘Dikteta’, ambayo imeanza kufanya vizuri
sokoni.
Filamu hiyo inayoonesha ukandamizaji wa familia,
imekamilika na kuingizwa sokoni hivi karibuni, ambapo tayari imeanza kufanya
vizuri katika mauzo baadhi ya maeneo ya
jijini Dar es Salaam, ikisambazwa na
kampuni ya steps Entertaiment.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Chekibudi
alisema, filamu hiyo ameiandaa ili kuonesha ukandamizaji uliopo baadhi ya
familia katika maisha ya kila siku, na amefarijika kuona iko katika wakati
mzuri sokoni.
Alisema baada ya kuangalia hilo, aliamua kuweka
wazo lake katika filamu ili kuwafikishia ujumbe watu wengi zaidi na ikawa kama
ni moja ya kazi za wasanii kuelimisha na kufundisha jamii.
“Unajua unapokuwa msanii unatakiwa kuwa mbunifu
katika mambo mengi na ndiyo maana kila kukicha tunaangalia ni jinsi gani
tutawakumbusha wenzetu matatizo ambayo yanaepukika,” alisema Chekibudi.
Chekibudi alishawahi kufanya vizuri alipokuwa
katika kundi la sanaa la ‘Splendid’, na katika filamu hiyo ya ‘Dikteta’ amewashirikisha
nyota wengine kama, Cojack, Philipo, Munira Sultan, Snura Mush, Coletha Reymond
pamoja na nyota wengine.
No comments:
Post a Comment