Na Bryceson Mathias
WAKATI Jeshi la polisi nchini, limewataka wananchi kutii sheria bila shuruti, na wasitumie mwanya wa makosa yanayofanywa na baadhi ya askari au wananchi wanaovunja sheria kuhalalisha uvunjafu wa sheria, ni mtazamo wangu Jeshi hilo lijitathimini.
Ingawa makosa mawili hayafanyi haki moja, ni rai yangu ieleweke kwamba, maonyo ya maneno ya Mungu Biblia Ezekiel. 16: 44- “Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake”, hivyo kama Polisi wanaotegemewa wanaongoza kwa kuvunja sheria, wananchi nao wataiga kuvunja.
Sikubaliani na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, anayenyoshea kidole kwa nguvu ubaya wa kutotii amri bila shuruti kwa wananachi pekee, bali nilitaka Polisi wanapokuwa vinala wa kuamua kuchukua sheria mikononi, adhabu yao iwe mara mbili kuliko wananchi ili tuikomeshe.
Hivi karibuni Senzo amelalamikia vitendo vinavyozidi kushamiri nchini kwa wananchi kuvamia vituo vya polisi, kuchoma moto vituo, au wananchi kuacha kabisa kutii amri halali za jeshi la polisi pindi askari wanapofika katika maeneo yenye fujo.
Kukikiri kwa Senzo kuwa ndani ya jeshi hilo kuna askari wachache wakorofi ambao sio waadilifu, hilo linadhihirisha kwamba, vurugu zingine za kutotii sheria bila shuruti, viranja wake wanakuwa askari wenyewe.
Wananchi wanapotakiwa kutii vivyo hivyo na Polisi wafanye hivyo, wasichukua mwanya wa wananchi kuhalifu na wao wenye ufahamu wa sheria wakalalisha, kujeruhi au kuvamia na kuleta taharuki na kusababisha Majeruhi na Ulemavu, ila watumie Taaluma kuepusha ili tujivunie wao.
Sikubaliani na tabia ya wananchi wanaovamina na kuharibu vituo vya polisi na wakati mwingine kuwaua askari au hata Raia. Nakubaliana kwamba watu wanaobainika kufanya hivyo wachukuliwe hatua kali ikiwezekana liwe fundisho kwa wanaoiga na kuendesha vitendo hivyo.
Ingawa nalipongeza Jeshi la polisi kwa kauli za kukataza uvunjaji wa sheria iwe ni kwa askari au raia, naomba makatazo hayo kwa askari yasiwe ya maneno au maandishi tu, bali yawe ya vitendo ili kuthibitisha kuwa, Polisi anapokosea anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za Jeshi sawa na raia.
Nasema hivyo kwa sababu katika nyakati fulani fulani, baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi wananchi wamewalalamikia kuwa wamekuwa sababu na vyanzo vya vurugu katika baadhi ya maeneo, kutokana na kuwataka wananchi watoe kitu kidogo wakati wa kutatua shida zao.
Wanadai, pindi wanapokataa kufanya hivyo, ndipo baadhi ya Polisi wasio waadilifu hutumia mwanya huo kuwabambikiza kesi zisizo za kweli, na kuwanyanyasa kwa kuwapiga kuwajeruhi na hata kuwaua, Jambo ambalo huamsha mtafaruku unaowafikisha kutotii sheria bila
shuruti.
Mimi naaamini kabisa, Watanzania ni watu wasikivu kama wakiongozwa kufanya mambo ambayo wanaamini kabisa hayana uonevu, na ndiyo maana wanakuwa wasamaria wema hata kuweza kutoa taarifa za uharifu unaotarajiwa kufanywa au unaofanyika mahali fulani fulani.
Lakini kinachoumiza, kuna miongoni mwa askari wasio waaminifu ambao hawana Kaba ya kichungaji shingoni, huamua kuwaambia waharifu kwamba, aliyetupa taarifa zako ni fulani na matokeo yake waharifu hao hujenga uadui na wananchi hao na kuhatarisha maisha yao.
Aidha kwa upande mwingine kinachowaudhi ni ambapo, wanatoa taarifa za uharifu wa mtu fulani na Polisi humkamata na kumfikisha korokoroni akiwa na vithibiti (Exibit vyote), lakini cha ajabu baada ya masaa, waharifu hao hukutwa wako nje wakiwataambia, na vithibiti vimetoweka. Hivyo ni rai yangu Jeshi lirudisha heshima yake kwa kufumuliwa.
No comments:
Post a Comment