HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2026

Tukio kubwa la kuibua vipaji vya Riadha laja Dar

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA) kinatarajiwa kuandaa tukio kubwa la mashindano ya kuibua vipaji kwa Vijana 'DAA Youth Talent Track and Field 2026' yatakayofanyika Machi 27 hadi 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za DAA zilizopo barabara ya Manispaa Temeke, Makamu Mwenyekiti wa DAA, Mwalimu Elizabeth Tungaraza, alisema kuwa watoto wanariadha 3,000 wenye umri wa miaka sita (6) hadi 17 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo, huku zaidi ya wazazi na wanajamii 10,000 wakitarajiwa kuhudhuria na kushuhudia tukio hilo.



Mwalimu Tungaraza, alisema mashindano hayo yanatajwa kuwa ya kipekee na ya kihistoria nchini Tanzania, yakilenga kuwa jukwaa kubwa la kitaifa la kubaini, kuendeleza na kulea vipaji vya watoto katika mchezo wa riadha.


“Mashindano haya yatazishirikisha shule, makocha, wazazi pamoja na wadau mbalimbali wa michezo kutoka pande zote za nchi,” alisema Mwalimu Tungaraza.


Alibainisha kuwa tukio hilo ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya riadha ya vijana kuwahi kufanyika nchini, likitoa mazingira salama, shindani na ya kuhamasisha yatakayowawezesha watoto kujenga na kuendeleza ndoto zao kupitia michezo.


Mbali na mashindano ya riadha, tukio hilo litapambwa pia na burudani mbalimbali pamoja na michezo ya kujifurahisha kwa watoto, hatua inayolenga kuwapa washiriki uzoefu wa kipekee, wa kuvutia na kuhamasisha ushiriki mpana wa jamii.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa DAA, Tullo Chambo, alisema mashindano hayo ni sehemu ya mfumo endelevu wa kuandaa wanariadha wa baadaye wa kitaifa na kimataifa.


Alisema kuanzishwa kwa kituo cha riadha, kutakuwa nguzo ya maendeleo endelevu, kitakachotoa mafunzo kwa vijana wenye vipaji pamoja na ufuatiliaji wa kielimu, kimwili na kisaikolojia ili kuhakikisha wanariadha hao wanakua kwa misingi imara.


“Kama sehemu ya utekelezaji wa maono ya muda mrefu, Dar es Salaam Athletic Association (DAA) inalenga kuanzisha Academy ya Riadha itakayokuwa nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya mchezo huu nchini Tanzania,” alisema Chambo.


Aliongeza kuwa Academy hiyo itatoa mafunzo endelevu ya kitaalamu kwa watoto na vijana waliobainika kuwa na vipaji kupitia mashindano na matukio mbalimbali ya riadha, sambamba na kuwaandaa kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages