HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 26, 2013

Swahili Tourism Fair kurindima Dar

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Balozi Charles Sanga (kushoto) na Ofiza Mtendaji wa Kampuni ya Witch & Wizard ya Afrika Kusini Zaida Enver wakisaini makubaliano ya kikazi baina yao ambapo kampuni hiyo kwa kushirikiana na TTB itaratibu maonyesho ya kimataifa ya utalii yanayojulikana kama Swahili Tourism Fair yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ni Mwanasheria wa TTB Ian Kaduma na Balozi wa Afrika Kusini nchini Thanduyise Chiliza (kulia)


DAR ES SALAAM, Tanzania

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yanayojulikana kama ‘Swahili Tourism Fair’ yanayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu chini ya uratibu wa Kampuni ya Witch & Wizard ya Afrika Kusini kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Akizungumza Dar es Salaam leo, Balozi wa Afrika Kusini nchini Thanduyise Chiliza alisema ushirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini katika Sekta ya Utalii utadumishwa zaidi ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la tiafa.

Balozi Chiliza aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano ya kikazi katika sekta hiyo kati ya pande hizo mbili ambapo kampuni mbalimbali kutoka maeneo tofauti duniani zinaalikwa kushiriki.
Alisema maendeleo katika sekta ya utalii yaliyofikiwa na nchi yake hayakuja kutoka mbinguni hivyo ilitoa wito kwa Tanzania kuendelea kufanya juhudi katika kuhakikisha inafikia maendeleo ya juu kwani ina rasilimali za kutosha  za kufanikisha malengo hayo.

“Mafanikio ya kimaendeleo mnayoyaona sasa nchini kwetu hayakuja kama muujiza, tumefanya kazi hivyo nanyi fanyeni kazi na mtafika pazuri kwani Tanzania ina rasilimali za kutosha kufanikisha malengo ya sekta hii” alisema Balozi Chiliza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa TTB Balozi Charles Sanga alisema maonyesho hayo ni fursa nzuri kwa Tanzania kuinuka kiuchumi kwani ushiriki wa kampuni utakuwa mkubwa na utatoa fursa kubwa kwa watanzania kufanya biashara.

Alisema pamoja na hilo sekta ya utalii nchini itakuwa na fursa ya kutosha kutangaza vivutio vyake ambapo ana imani baada ya maonyesho hayo Tanzania itaongeza idadi ya watalii watakaoingia nchini.
Ofisa Mtendaji wa kampuni ya Witch & Wizard Zaida Enver alisema watahakikisha ushiriki wa kampuni za kitalii unakuwa mkubwa katika maonyesho hayo ambapo kuanzia sasa watatoa fursa kwa kampuni kote duniani kujisajili kwajili ya ushiriki.

Alisema wamefikia maamuzi ya kufanya kazi na Tanzania baada ya kuona mafanikio ya ushiriki wa TTB katika maonyesho mbalimbali likiwemo lile la Indaba Tourisim Fair linalofanyika nchini Afrika Kusini chini ya uratibu wao ambapo Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi bora zenye vivutio vingi vya utalii.
Maonyesho hayo yanatarajiwa kufanyika nchini katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam kuanzia Oktoba 2 hadi 5 mwaka huu ambapo pamoja na maonyesho kutakuwa na kongamano la wafanyabishara washiriki litakalolenga kubadilishana uzoefu. 

1 comment:

  1. Hii ni wazo zuri nasi tuoneshe jinsi gani tumeiva kwa kuandaa maonesho ya kitalii,kama miundo mbinu tunayo ya kutosha sasa why not!big up TTB.

    ReplyDelete

Pages