HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 26, 2013

Tamasha la Pasaka kuvuruga Dar hadi Musoma kwa siku 10


 Na Elizabeth John

TAMASHA la Pasaka mwaka huu linatarajiwa kufanyika kwa siku nane mfululizo kuanzia Machi 31 hadi Aprili 7 katika mkoa saba, ikiwa ni mara ya kwanza tamasha hilo kufanyika mikoa zaidi ya mitatu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, wamefanya hivyo kwa kuheshimu maoni ya wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili, ambao kwa kuguswa na tamasha hilo, wameomba kufikiwa ili kuzoa baraka za Mungu ambazo huambatana na ujumbe wa nyimbo mbalimbali kutoka kwa waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania.

Msama alisema kuwa, maadamu kamati yake imeridhia maombi ya kuongeza idadi ya mikoa, wanawasihi wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili katika mikoa ambayo Tamsha litafika, kujitokeza kwa wingi kujionea na kuchota baraka za Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo na hakuna atakayejutia muda wake wa kwenda kulishuhudia.

Mikoa rasmi iliyoshinda katika kivumbi cha uwenyeji wa tamasha hilo ni Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza na Mara, ambayo imepatikana baada ya wapenzi, mashabiki na wadau kupiga kura kwa njia ya simu na kilichobaki sasa ni Kamati ya maandalizi kutimiza ahadi yake ya kuwapelekea uhondo huo wa muziki wa injili.

Msama alifafanua kuwa, baada ya Tamasha hilo kuzinduliwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 31, siku itakayofuata litakuwa Uwanja wa Sokoine Mbeya kabla ya kutua Uwanja wa Samora, Iringa Aprili 3 na Aprili 6, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma na siku itakayofuata kishindo cha tamasha hilo kitatua CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Alisema baada ya kuvuruka kwenye mikoa hiyo, tamasha hilo litaelekea Musoma na Tarime kwa ajili ya kuhitimisha tamasha hilo ambalo limezidi kupata umaarufu mkubwa kutokana na maudhui yake, ambako safari hii limebeba ujumbe wa kuhamasisha suala la Amani na Upendo kwa watu wote bila kujali kabila, dini wala itikadi.

No comments:

Post a Comment

Pages