HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2013

UKATILI UNAWAOGOPESHA WANAUME KUOA NA WANAWAKE KUOLEWA.

Adha ya Unyanyaswaji Mama huyu asiyejulikana jina aliyekutwa na Mwansishi mkoani Dodoma usiku akiwa amelala kwenye ukuta wa Jamatin.
 
Na Bryceson Mathias

VITENDO vya Ukatili vinavyofanywa na wanandoa dhidi ya unyumba wao, hivi sasa vimekuwa vikiwaogopesha wanaume na wanawake walio wengi kuogopa kuoa au kuolewa, hasa mijini tofauti na vijijini ambako wakati mwingine watu hulazimishwa na mila na desturi.

Ingawa kuna ukweli usiopingika kwamba, Nyumba hujengwa kwa hekima, kuimarishwa kwa busara, maarifa na vyumba vyake kujazwa na vitu vya thamani kama upendo vyenye kuimarisha nyumba, bado  hekima ya dunia imepata nafasi kuharibu tunda la roho zikiwamo ndoa.

Maandiko Katika Biblia Mithali 24:3-4; ” Nyumba hujengwa kwa hekima, na kuimarishwa kwa busara.kwa maarifa na vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza”

Lakini nyakati hizi, Ukatili wa wanaume na wanawake mara baada ya ndoa, hivi sasa umeonekana kushamili nchini, ambapo huwaumiza wanawake na wanaume kwa upande mwingine na kuwafanya waogope kuoa na kuolewa.

Ingawa Mwanamke ni nguzo kubwa na muhimu sana katika maisha na maendeleo ya mtu binasfi, jamii na taifa kwa ujumla. Mwanamke ndiye nguzo katika uzalishaji na ujenzi wa taifa katika kuongeza rasilimali watu na pato la taifa katika nyanja za uchumi hasa kilimo, Mafanikio yoyote yanayopatikana, basi nyuma ya mafanikio hayo lazima wapo wanandoa.

Mwanamke ndio mlezi mkuu wa familia na jamii. Jamii inapokuwa na maadili mema basi juhudi na kazi kubwa imefanywa na mwanamke akishirikiana na mwanaume.

Licha ya umuhimu mkubwa alionao mwanamke katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, jamii na Taifa; Mwanamke hapewi umuhimu mkubwa katika jamii hasa katika mtazamo wa usawa.

Siku zote tunaamini kuwa binadamu wote ni sawa kati ya mwanamme na mwanamke., lakini mtu awaye yote atatarajia kuona mwanamke anachukua asilimia kubwa ya kunyimwa haki, iwe kwa muewe hata kwa familia, ingawa Serikali za kiafrika ndiyo kwanza zimeanza kuzinduka.

Ukatili mkubwa unaofanywa siku hizi ni ukatili dhidi ya wanawake. Ukatili huu kwa kiasi kikubwa humuathiri sana mwanamke Kimwili, Kiroho na kisaikolojia.

Hivi karibuni vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vimeshamiri kwa kasi ya ajabu. Vitendo hivi vya ukatili ni pamoja na kupigwa, udhalilishaji toka kwa wanaume, ubakaji, ndoa katika umri mdogo, ukeketaji na ajira za utotoni.

Vyama mbalimbali vya wanawake Tanzania vinapigania sana kutokomeza unyanyasaji, udhalilishaji na ukandamizaj wa wanawake. Vyama hivyo ni kama TGNP, TAWLA, TAMWA na vinginevyo vinapigania sana haki ya kikatiba ya ibara ya 12 hasa ibara ndogo ya 2 inayosisitiza stahili ya heshima na kutambuliwa utu wa kila mtu hasa haki ya mwanamke na mtoto.

Mama mmoja Mkazi wa Mbulu wilayani Babati mkoani Manyara, ni mmoja wa waathirika wa ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Alipatwa na mkasa wa kugongwa na gari na mumewe na kisha kufungwa chini ya gari na kuburuzwa umbali wa kilometa 1 mpaka mahali panapofahamika Sokoni.

Mama huyu alipata madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuvunjika mguu, kuvunjika mbavu saba na majeraha makubwa mgongoni yaliyotokana na ngozi yote kutoka mpaka kusababisha nyama na mifupa ya ndani kuonekana.

Huu ni ukatili uliopitiliza ambao haulingani na kosa lolote kustahili adhabu kama hiyo kwa binadamu mwingine. Hii yote inatokana na mfumo dume unaoamini kuwa ukioa mke ni mali yako na unaweza kumfanyia chochote juu yake, na hali hii ndiyo ambayo inawafanya sasa waogope kuolewa.

Ukatili kama huu ulitokea huko nyuma mkoani Mara, ambapo mwanamke mmoja alipigwa na mumewe na mchi wa kinu na kumvunja kabisa miguu yake  miwili, lakini mpaka taarifa yake inatolewa kwa umma, tayari alikuwa ni kilema asiye na miguu na wakati mwingine watuhumiwa hao kutochukuliwa hatua yoyote.

Kisa kifananacho na hiki kilitokea pia Kilosa mkoani Morogoro ambapo mwamume alimcharanga mkewe mapanga manne sehemu ya kichwa na mgongo. Watendaji wa makosa haya wote hukimbia baada ya kutenda makosa haya na kuona kuwa hatua za dhati zinachukuliwa juu yao.

Dhana ya ukeketaji katika maeneo kadhaa ya mila na desturi kwa makabila fulani nchini, limkuwa ni kadhia kwa wanawake katika baadhi ya Vitongoji, Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na mikoa, ambapo wakikutwa hawajakeketwa, huwa na misuguano kwenye ndoa na kulazimishwa kufanywa hivyo, ambapo wengine hupoteza maisha ukubwani, vipigo vikiongoza hali inayowafanya wanawaka wapate uoga wa kuolewa.

Ni Rai yangu kwa serikali, ihakikishe inachukua hatua mbalimbali za kukomesha aina zote za ukatili dhidi ya wanawake  pamoja na watoto,  kwa kuweka sheria mpya na kuzirekebisha zilizopo ambazo hazionekani kukidhi haja  kwa wakati uliopo, ili kuwanusuru wanawake.

Njia nyingine ni kuwapa wanawake nguvu kubwa ya kiuchumi na maendeleo ikiwa ni pamoja na kuzipa msukumo wa kipekee Jumuia  na Asasi zisizo za kiserikali zinazojitokeza kukokomesha uovu dhidi ya wanawake na watoto ,na kujenga mazingira yao  ya kukuza maendeleo na kulindwa.

No comments:

Post a Comment

Pages