HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 13, 2013

YANGA WAWAPANIA AFRICAN LYON UWANJA WA TAIFA LEO

 Kikosi cha Yanga
 Kikosi cha African Lyon
 Wachezaji wa Yanga na African Lyon wakiingia dimba la Taifa katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ambayo Yanga ilishinda kwa mabao 3-1. Mechi hiyo ilichezwa Septemba 11, 2012.
Ni moja ya hekaheka wakati wa pambano la Yanga na African Lyon kwenye dimba la Taifa katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ambayo Yanga ilishinda kwa mabao 3-1. Mechi hiyo ilichezwa Septemba 11, 2012.
 Logo Yanga
Logo African Lyon

DAR ES SALAAM, Tanzania

Mechi nyingine za Ligi Kuu zitakazopigwa leo ni kama ifuatavyo: Toto Africans watakuwa nyumbani CCM Kirumba kuwaalika Polisi Morogoro, Mgambo watakuwa Mkwakwani kucheza na JKT Oljoro, huku Mtibwa Sugar ikiwaalika Ruvu Shooting huko Manungu Complex

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo wanashuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuumana na waburuza mkia wa ligi hiyo African Lyon, huku wakipania kushinda ili kutanua wigo wa pointi kwenye msimamo wa ligi iliyo katika mzunguko wa lala salama.

Yanga inayoongoza ligi ikikabwa koo na ‘Wana Lambalamba’ Azam FC zote zikiwa na pointi 33 na kutofautishwa na uwiano wa mabao, leo imepania kuichapa Lyon, ili kupanua wigo wa pointi dhidi ya ‘Vijana wa Chamazi’ wanaotishia uongozui wao.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame,’ wanajitupa dimbani wakitarajia kumkosa beki wake mahiri Mbuyu Twite ambaye ni majeruhi – anayetajwa kuweza kuiathiri Yanga katika jaribio la kuikimbia Azam.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema maandalizi ya pambano dhidi ya Lyon yameenda vizuri na kwamba hakuna ongezeko la majeruhi, kitu kinachompa kocha wigo mpana wa kupanga kikosi chake.

“Kikosi kiko sawa kabisa kuelekea mechi hiyo na hakuna ongezeko la majeruhi zaidi ya Twite, ambaye hata hivyo kocha anatambua namna ya kujaza pengo lake, kwani ana wigo mpana wa kupanga kikosi. Mashabiki waje kwa wingi kusapoti kikosi chao,” alisema Kizuguto.

Aliwatoa shaka mashabiki hao wa Yanga kutokana na ushindani uliopo dhidi ya Azam FC na kuahidi kuwaacha pointi tatu nyuma kwa kushinda mchezo wa leo: “Nia ya kila timu ni kushinda mechi, nasi tumejiandaa kwa hilo na mashabiki hawapaswi kuihofia Azam,” aliongeza.

Yanga inashuka dimbani leo ikitoka kuambulia sare ya bao 1-1 ilipoumana na Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, huku Lyon ikitoka kuchapwa mabao 2-0 na Tanzania Prisons katika mechi iliyopita kwenye dimba la Sokoine, Mbeya.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Septemba 30 mwaka jana, Yanga iliizabua Lyon kwa mabao 3-1 na leo itapania kuendeleza ubabe, huku Lyon ikitaka kufuta uteja.

Mechi nyingine za Ligi Kuu zitakazopigwa leo kwenye viwanja tofauti ni kama ifuatavyo: Toto Africans ‘Wana Kishamapanda’ watakuwa nyumbani CCM Kirumba kuwaalika Polisi Morogoro, Mgambo watakuwa Mkwakwani kucheza na JKT Oljoro, huku Mtibwa Sugar ikiwaalika Ruvu Shooting huko Manungu Complex.

No comments:

Post a Comment

Pages