Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen akiwaonesha waandishi wa habari timu wanazocheza wachezaji wa Morocco katika vialabu vya Ulaya. (Picha na Habari Mseto blog)
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen akifafanua jambo wakati akitangaza kikosi cha wachezaji 23 watakaoingia kambini kwa ajili ya mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakaofanyika mwakani nchini Brazil.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji 23 watakaoingia kambini Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya mashindano dhidi ya Morocco.
Mechi hiyo ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma, Machi 17 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA KUFANYIKA MACHI 19
Semina elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013 itafanyika Machi 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) siku moja kabla (Machi 18 mwaka huu).
Washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment