Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),
imekamata magari 144 ya abiria kutokana na kufanya makosa mbalimbali.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Mfawidhi
Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shiyo, alisema magari hayo yamekamatwa
kuanzia mwanzoni mwa wiki hii.
Alisema kati ya magari hayo 63 yaliokamatwa ni kutokana na makosa
ya kuwatoza abiria nauli kinyume na ile elekezi, kutumia tiketi za zamani na kukatisha njia
huku wakijua fika kuwa kufanya hivyo ni kosa.
“Tumegawa chati za bei kuanzia Jumatatu kwa kila gari, zenye
utambuzi wa bei ya nauli za zamani na mpya hivyo kila mwananchi anayo haki ya
kuoneshwa chati hiyo pindi anapotaka na akinyimwa kuiona hilo ni kosa na
mhusika atachukuliwa hatua,”alisema Shio.
Aliyataja makosa mengine kuwa ni pamoja na magari 71 ambayo
madereva na makondakta wake walikutwa wakiwa hawakuvaa sare za kazi na matumizi
ya lugha chafu kwa abiria ambako adhabu za makosa hayo faini zake zinaanzia sh
100,000 na kuendelea.
“Nawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha
operesheni hii ya kukamata magari haya,
tunawaomba waendelee kutuletea taarifa za madereva hao ili tuweze kuwashinda
wakorofi hawa wasiotaka kutii sheria za nchi”alisema Shio.
Shio alitoa wito kwa abiria kuwa wasikubali kulipa nauli na wahakikishe
kuwa wanalipa nauli halali, pia ni aibu kwa abiria hao zaidi ya 31 kushindwa na
watu wawili yani kondakta na dereva wake
kwa kuwaarisha wanavyotaka.
Katika hatua nyingine Sumatra imetangaza njia mpya ya
Mbezi/Ubungo Maziwa na Tegeta/ Ubungo Maziwa lengo za njia hizo ni kwa ajili ya
kuwasaidia abiria wanaoishia kituo cha treni ya masafa mafupi Ubungo.
Shio aliwataka wamiliki wote wanaotaka kusajili magari kwa ajili
ya njia hizo zilizotajwa hapo juu wanakaribishwa.
Aliongeza kuwa barabara zitakazotumika watajulishwa wakati wa
maombi ya leseni ya biashara (TLA).
No comments:
Post a Comment