HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 30, 2013

Ndugulile CCM, Kama Mpinzani, akataa kutishiwa Nyau!


 Na Bryceson Mathias
KAMA kuna Mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anayetakiwa kupokewa Kishujaa akirudi jimboni kwake toka bungeni kana kwamba ametoka vitani na ameshinda vita; basi ni Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustine Ndugulile.
Sababu zinazomfanya Mbunge Ndugulile apokewe kishujaa na wananchi wake jimboni si ngeni bali ni ile aliyowahi kusema awali kwamba, Yuko tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Jimbo lakela Kigamboni si wapiga kura tu.
Safari  hii Ndugulile, akiwa na sura inayompendeza kuwa Mpinzani alithubutu kukataa ambazo yeye aliziita Porojo za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Prof. Anna Tibaujuka na Wizara yake akipinga wananchi wake wa Kigamboni kutofaidika na Mradi wa Makazi Mapya na kuingia mitini kwenye kikao.
Ikikumbukwa April 8, mwaka huu Dk. Ndugulile, aliapa kuwa yupo tayari kufa kwa ajili ya wananchi wa Kigamboni na haogopi vitisho vya baadhi ya wana CCM wanaohoji uhalali wa uanachama wake, kwa kile kilichoonekana na kuwatetea wananchi wake.
Alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika uwanja wa Swala, Kigamboni jijini Dar es salaam, Mbunge huyo alisema vitisho vya watu hao vinatokana na hatua yake ya kupinga dhuluma katika mradi wa mji mpya wa Kigamboni.
Dk. Ndugulile alisema kamwe hawezi kuzibwa mdomo kwa kuwatetea wananchi wake waliompigia kura na kumuamini na aliongeza kuwa ana uwezo wa kuwatetea na kuwaletea maendeleo ndani ya jimbo hilo, hata kama kuna watu wanasema, “Ukitaka Ubaya nchini Tanzania dai haki yako Uone!”
siku hiyo ambayo alihutubia kwa staili ya kuwauliza maswali wananchi, Mbunge huyo alisema wananchi wa Kigamboni bado hawajaelewa mambo muhimu katika mradi huo na ndiyo maana kila anapowauliza kama wanafahamu mradi huo lini utaanza, sehemu utakapoanzia na kiasi cha fidia, hawakuwa na majibu.

alisema "Angalieni wenyewe, nimewauliza maswali lakini hakuna jibu, hata mimi pia sijui kwa sababu sina nyaraka zozote zinazoonyesha vitu hivyo,"
Aliongeza kusema maswali kama hayo amewauliza viongozi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi akiwamo Waziri Profesa Anna Tibaijuka, lakini cha kusikitisha wote hawakufahamu.
"Sipo hapa kupinga mradi wa mji mpya, ninayosema ndiyo maneno yenu ninyi wana-Kigamboni, sasa asiwepo mtu akaanza kupotosha na kuniona mimi napinga Ilani ya Chama changu," alisema.
Hata hivyo, alisema tayari suala lote la mji mpya wa Kigamboni alilipeleka katika vikao vya Chama ili kujadiliwa kwa umakini, ambapo aliwataka wananchi wake kusubiri uamuzi wa vikao hivyo
hata hiyo alizungumzia fidia ya Sh. milioni 145 kwa ekari iliyotangazwa na Waziri Prof. Tibaijuka, ambayo Dk. Ndugulile alisema fidia hiyo ni kiini macho kwa sababu wakazi wengi wa Kigamboni hawana maeneo yenye ukubwa kama huo
Nanukuu "Sisi wakazi wa Kigamboni tunaishi watu ishirini ndani ya ekari moja, sasa ukigawanya kiasi hicho kwa idadi hiyo, ni wazi mwananchi wa kawaida hatapata fidia inayolingana na thamani ya eneo lake. Hii ni kutudanganya tu," aliongeza
Siku hiyo hiyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Yahaya Sikunjema, bila kumung’unya maneno aliwaambia wanachama wa CCM kuwa Mbunge huyo kijana, ni mwanachama mtiifu wa CCM na hawezi kuondoka kwenye chama hicho hata kama kuna watu wenye nia mbaya wanataka afanye hivyo.
Sikunjema alidai kama mivutano ilitokana na uwepo wa mradi wa mji mpya wa Kigamboni, hivyo chama hicho kiliamua kuingilia kati kujadili changamoto mbalimbali zilizoukabili mradi huo
Katika kujadili makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi iliyowasilishwa na Prof. Tibaijuka, Ndugulile alimshambulia waziri akisema anatoa porojo kwamba yeye (Ndugulile) aliingia mitini katika kikao cha madiwani ambapo ukweli halisi alikuwa safari ya kikazi.
Aidha Pamoja na Spika Anne Makinda kujaribu kumtisha Ndugulile ili alainike au kuogopa asiendelee kuwatetea wananchi wa Kigamboni, Mbungu huyo Kijana alikataa kutishiwa Nyau na kuendeleza mapambano hadi Spika akalazimika kuitaka Serikali ikake na wananchi wa Kigamboni iridhiane nao.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308

No comments:

Post a Comment

Pages