Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Udalali ya Flamingo, Nyalila Noel akipandika hati ya mahakama katika basi la Shirikisho la soka Tanzania (TFF), ambayo inaruhusu kukamatwa kwa mali za shirikisho hilo.
Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Udalali ya Flamingo, Nyalila Noel akibandika hati ya mahakama katika basi la Shirikisho la soka Tanzania (TFF), ambayo inaruhusu kukamatwa kwa mali za shirikisho hilo.
Dereva la basi dogo la TFF (kulia), akisoma hati ya mahakama iliyotolewa kwa ajili ya kukamatwa kwa mali za TFF kutokana na deni la sh. milioni 51 linazodaiwa na Safina Holding.
Hati ya mahakama.
'Sasa tunafunga na kuondoka nalo'.
Wafanyakazi wa Jay Ambe Break Dowan wakichakalika na ufungaji wa basi la TFF tayari kwa ajili ya kuondoka nalo kutokana na deni wanalodaiwa na Safina Holding.
Gari dogo aina ya Toyota Crown lenye namba T 643 BJW likiwa limezuia gari la Jay Ambe Break Down lisitoke katika lango kuu la kutoka na kuingia katika Ofisi za TFF, baada ya mali za shirikisho hilo kukamatwa na dalali wa mahakama.
Hati ya kukamata mali za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikiwa imebandikwa katika basi kubwa aina ya Youtong kwa ajili ya utekelezaji
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah akizungumza na waandishi wa habari wakati wa sakata hilo.
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), leo umejikuta kwenye wakati mgumu baada ya madalali wa Kampuni ya Flamingo Auction Mart, kutinga katika ofisi za shirikisho hilo na kukamata baadhi ya mali zake ili zipigwe mnada kufidia deni wanalodaiwa.
Shirikisho hilo linadaiwa na Safina Holding ya jijini Dar es Salaam zaidi ya sh milioni 50, baada ya kuwaweka katika hoteli ya kampuni hiyo maeneo ya Kijitonyama, waamuzi wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012.
Sakata hilo liliweza kudumu kwa muda wa saa nne kuanzia saa tano asubuhi na kudumu hadi saa tisa mchana, baada ya TFF kukubali kulipa sh milioni 20 kati ya sh 51,507,012 zilizokuwa zikidaiwa.
Awali, madalali hao wa Flamingo, walifika Ofisi za TFF, Karume Ilala na kujadiliana na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah na kushindwa kufikia muafaka, hali iliyowalazimu kuita gari maalumu ‘break down’ mali ya Jay Ambe na kulifunga basi dogo aina ya Toyota Coaster.
Baada ya gari hilo kufungwa ili likokotwe kupelekwa ‘yadi’ ya Flamingo, mlinzi wa TFF aliamua kukimbilia geti la kutokea na kulifunga na kuwafanya madalali hao washindwe kutoka nalo.
Jambo hilo lilizidisha sintofahamu na kuwafanya baadhi ya watu kuingia ndani kushuhudia kinachoendelea, huku maofisa wa Flamingo wakihangaika kuwasiliana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kuweza kutekeleza amri ya mahakama.
Usumbufu huo wa kuzuia madalali wasitekeleze amri halali ya mahakama, ulisababisha kero kwa watu mbalimbali waliofika Karume, kwa kushindwa kuingia ama kutoka katika ofisi hizo.
Wakati majadiliano yakiendelea, zilipatikana taarifa kuwa TFF wameomba walipe sehemu ya fedha wanazodaiwa kwa ahadi ya kumalizia zilizobaki, ili magari yake yasichukuliwe, hali iliyomfanya dereva wa gari lililozuia mlango kwenda kuliondoa na kuruhusu shughuli zingine kuendelea.
Ilipofika saa tisa mchana, Osiah alijitokeza na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa wamemuagiza mhasibu akachukue fedha benki.
Akizungumzia adha hiyo, Osiah alisema wao hawakujua kama tukio hilo litatokea, kwa kuwa barua waliyokuwa nayo haikueleza hivyo, na kudai kushangazwa na hatua hiyo, wakati barua kutoka Flamingo ikionekana kuchanganya tarehe ya zoezi hilo kufanyika.
Osiah alisema walipata nguvu za kugoma magari hayo yasichukuliwe kutokana na kugundua kuna makosa ya tarehe katika barua hiyo, huku akikiri kudaiwa sh milioni 28.
“Sisi tunadaiwa mil 28/-, ila mambo ya kimahakama ndio maana ikafikia hiyo na pia tumewashangaa sana Safina, badala ya mambo tuyamalize wenyewe, wao wanayakuza na fedha hizo zilitokana na hifadhi ya waamuzi katika michuano ya Chalenji,” alisema Osiah.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Flamingo, Deogratius Luziga, alisema wao walifikia hatua hiyo ya kutaka kuondoka na magari hayo kama amri ya mahakama ilivyowaagiza na kudai kuwa tatizo kubwa ilikuwa ni dharau za Osiah na kuwa angefanya hivyo toka awali wasingechukua muda wote huo katika zoezi hilo.
“Tumekubaliana mara baada ya kutuomba sana, tumekubali watangulize milioni 20/- kwanza, halafu milioni 31/- watamaliza ndani ya siku 14, kwani hii mahakama inaruhusu na bila hivyo, tutafanya kama tulivyokusudia kwa kuwa bado ni mali yetu sisi,” alisema Luziga.
Awali, Osiah alionekana kuchanganyikiwa na kuwasihi madalali hao kuachana na zoezi hilo la kuchukua magari hayo.
“Naombeni muache kufanya hivyo ambavyo mnataka kufanya, mimi sasa hivi namwambia mhasibu wetu mwende naye benki akawape fedha zenu zote jamani, msifanye hivi,” alisihi Osiah.
No comments:
Post a Comment