HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 22, 2013

Kinondoni yajichanganya yageuza barabara kuwa eneo la wazi

Na Mwandishi Wetu

MANISPAA ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imejikuta ikiwa katika wakati mgumu, kutokana na kitendo cha kuligeuza eneo la barabara kuwa eneo la  wazi na kuiruhusu Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, kuliboresha kwa ajili ya kulifanya kuwa maegesho ya magari kinyume na taratibu za mipango mji.

Eneo hilo lililopo Tindiga mtaa wa Mikocheni ‘ A’, kiwanja namba 269, 270, 271 na 272, linadaiwa kuwa ni sehemu ya barabara ambayo inaanzia nyuma ya Shule ya Awali ya Feza, inayopita Nyumbani kwa Rais Ally Hassan Mwinyi na kutokezea Kawe.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ya Machi 8, 2013 na kusainiwa na Mhandisi wa Manispaa hiyo Injinia Uriyo G. A, imeonyesha kwamba mwekezaji ameruhusiwa kuboresha eneo lililo nyuma ya Kiwanja namba 270, kama eneo la wazi.

Barua hiyo inaeleza kuwa eneo hilo ni la wazi, hivyo linabaki kuwa mali ya Manispaa na kwamba litakapohitajika kwa matumizi ya umma, litatakiwa kuachiwa bila ya pingamizi.
Hata hivyo, barua hiyo inafafanua kuwa gharama za kuboresha eneo hilo kwa mujibu ramani iliyowasilishwa na mwekezaji huyo zitakuwa juu yake na haruhusiwi kujenga ‘structure’ yoyote ndani ya eneo hilo la wazi.

“Kabla ya kazi kuanza na wakati kazi ikiendelea mwekezaji anatakiwa kuwasiliana na ofisi ya Mhandisi wa Manispaa kwa ukaguzi na ushauri,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Aidha, imeelezwa kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mwekezaji huyo, amejenga ukuta ambao umeziba barabara hiyo kuanzia upande wa kutokea shule ya Feza, kiwanja namba 269 na upande wa pili wa kuelekea kwa Rais mstaafu Mwinyi Kiwanja namba 272 kinyume na maombi yake ya kuboresha eneo la wazi lililo nyuma ya kiwanja namba 270.

Barua ya maombi iliyosainiwa na Ephraem Mrema  kwa niaba ya Trans Auto Express Ltd, inaonyesha kwamba Kampuni hiyo ni ya wazalendo na inamiliki kiwanja namba 270 Keko Avenue, Mikocheni ambapo hapo awali waliipangisha nyumba hiyo kwa shirika la Kimataifa la Misaada Oxfam na baadaye Taasisi ya Moyo (Tanzania Heart Institute).
Barua hiyo inaendelea kusema kwamba nyuma ya eneo hilo upande wa mashariki kuna eneo la Tindiga ambalo kwa muda wote limetelekezwa siyo tu na wote walio na viwanja vinavyopakana na eneo hilo bali pia na Manispaa ya Kinondoni.

Hata hivyo, barua inaonyesha kuwa Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, imeiomba Manispaa kibali cha kuliboresha eneo hilo la wazi kwa kulisafisha, kuchimba na kutupilia mbali udongo wa juu kwa kina cha mita moja, kuweka mawe na tabaka gumu (base course), kusindika na kuweka paving blocks pamoja na mifereji ili kutoa maji na kuyapeleka kwenye mkondo wake wa asili.

Kwa mujibu wa barua hiyo eneo linaloombwa lina ukubwa wa takribani mita za mraba 2,300, wamekadiria kuwa litawagharimu kiasi cha shilingi milioni 200 kwa kazi za awali na shilingi milioni 12 kila mwaka kwa ajili ya kulitunza.

Hata hivyo, vyanzo vyetu vimebaini kwamba kuna makubaliano mengine ya malipo ya kila mwenzi kwa mwekezaji kuilipa Manispaa shilingi milioni 1,960,000 kama kodi ambayo haijabainishwa katika barua ya  Manispaa kumjulisha mwekezaji.

Baadhi ya majirani wa eneo hilo wanahoji ni kwa vipi mwekezaji huyu atumie zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuliboresha eneo hilo tu na shilingi milioni 12 kila mwaka kulitunza na milioni 1, 960,000 kila mwenzi kama kodi.

Majirani hao wanahoji, iweje Manispaa iruhusu Kampuni mmoja kulipatia eneo hilo kwa ajili ya kuliboresha, wakati kama ingetoa ruhusa ya kila mwenye nyumba afanye maboresho ingewezekana na wangeweza kuilipa Manispaa shilingi 100,000  kwa kila Nyumba kwa mwenzi na wangeweza kusanya shilingi 400,000  kwa mwenzi, tofauti na mwekezaji huyo anayelipa shilingi 163,000 kwa mwenzi.

Vyanzo vyetu, vimebaini kwamba hakuna makubaliano ya mkataba ulioingiwa baina ya Manispaa ya Kinondoni na mwekezaji Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, juu ya masharti waliyopeana, na wala hakuna majibu ya barua ya Machi 8, 2013 ya kukubali masharti waliyokubaliana.
Inasemeka kwamba mradi huo umewashirikisha mmoja wa kigogo wa cheo cha juu wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA na mwinge wa ngazi ya juu wa serikali, jambo ambalo limepelekea Manispaa kukubali kwa urahisi sana kulitoa eneo hilo la barabara na kuligeuza eneo la wazi na kuiruhusu Kampuni hiyo kuliboresha kwa ajili ya matumizi yake wanayotalajia.

Kampuni hiyo Trans Auto Express Ltd ina husika na kupakua na kupakia mizigo inayoingia na kutoka nje ya nchi (clearing na forwarding).

Uchunguzi wetu, umegundua kuwa eneo hiyo linataka kugeuzwa kuwa sehemu ya kuhifadhia makontena na magari madogo yatakayoingizwa nchini na mingine ya nchi za jirani yanayotolewa bandarini ambayo yatahifadhiwa mahali hapo.

Alipotafutwa Ephraem Mrema ili kutoa ufafanuzi kuhusu barua ya maombi kwa niaba ya Kampuni ya Trans Auto Express Ltd,  alisema kuwa hausiki na kitu chochote kwa maelezo zaidi afutwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

“Mimi sihusiki na kitu chochote nimeshamalizana na watu wa Manispaa na wala mimi siyo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ni mwajiliwa tu kama anavyo ajiliwa mtu yeyote yule” alimaliza kusema Mrema.
Mwandishi wetu alipowasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mussa Natty, amewataka viongozi wa serikali ya Mtaa wa Mikocheni, wilaya ya Kinondoni kusimamia sheria za ujenzi katika maeneo mbalimbali ili kuepuka migogoro kati ya wananchi na serikali.

Natty alisema kuwa watendaji hao hawapaswi  kukaa kimya pindi wanapobaini mwekezaji akijenga katika maeneo ya wazi ama ya barabara kwa matumizi yake binafsi, kwa kuwa sheria zipo wazi na kila mmoja anapaswa kuzitii bila shuruti.

Mkurugenzi huyo aliendelea kusema kuwa iwapo kuna yeyote aliyejenga katika eneo la wazi na kusababisha adha kwa wengine, ni muhimu watendaji wakachukua hatua kutokana na mwekezaji huyo kuvunja sheria.

No comments:

Post a Comment

Pages