Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Promotions, Alex Msama.
Na Francis Dande
Mkurugenzi Mtendaji wa Msama
Promotions, Alex Msama, amemkabidhi msaada wa magodoro yenye thamani ya sh.
milioni 4.5 mlezi wa kituo cha watoto yatima cha Luhila Pachane kilichopo
Songea mkoani Ruvuma, Sheikh Abdushakur Omary. Hafla hiyo ilifanyika leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis
Dande)
Na Francis Dande
MKURUGENZI Mtendaji wa
Msama Promotions, Alex Msama, amekabidhi msaada wa magodoro yenye thamani ya
zaidi ya sh milioni 4 kwa kituo cha watoto yatima Luhila Pachane kilichopo
Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo makao makuu ya ofisi za Msama Promotions, Kinondoni jijini Dar es
Salaam jana, Msama alisema msaada huo umetoka kwenye Mfuko wa Tamasha la
Krismasi ambalo linatarajiwa kuanza Desemba 25 jijini hapa na mikoa mingine.
Tamasha hilo linatarajia
kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Arusha na Dodoma.
Msama alisema kuwa kutokana
na maombi ya kituo hicho na kuguswa na hali waliyokuwa nayo ya yatima hao
kulala katika mikeka, aliamua kunyofoa sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye Mfuko
wa Tamasha la Krismasi na kuwasaidia watoto hao ili nao waweze kujisikia wapo
katika jamii ya Watanzania.
“Nimeamua kufanya hivyo
kutokana na kuguswa na hali halisi waliyonayo yatima hao wa kituo cha Luhila
Pachane huko mkoani Ruvuma, nikaamua kunyofoa fedha katika Mfuko wa Tamasha la
Krismasi kwa ajili ya kuwasaidia ili nao wajisikie wako pamoja na Watanzania
wenzao.
“Msaada huo wa magodoro
hayo ni zaidi ya shilingi milioni 4, hivyo nina imani kubwa sasa kwa msaada huu
yatima wataniombea kwa Mungu ili Tamasha la Krismasi liwe la mafanikio, kwani
lengo la tamasha hilo ni kuweza kujenga kituo cha kisasa cha watoto yatima na
wasiojiweza, kwani kiwanja tumeshakiona kipo pale maeneo ya barabara ya Pugu jijini
Dar es Salaam,” alisema Msama.
Akizungumza baada ya
kukabidhiwa msaada huo, mlezi wa kituo hicho ambaye pia ni Katibu wa Bakwata
Mkoa wa Ruvuma, Sheikh Abdushakur Omary, alimshukuru Msama kwa wema wake
aliouonyesha wa kusaidia jamii ya Watanzania wote bila kubagua dini, kabila
wala rangi.
“Msama ni mtu wa aina yake,
hana ubaguzi, anashughulikia maombi ya Watanzania wote bila kuangalia dini,
kabila, rangi wala utaifa wake, kwani anaamini kuwa wote ni wamoja, hivyo
naomba tuzidi kumuombea aendelee kuwa na moyo huo wa kujitolea kwa ajili ya
watu wa taifa lake wasiyojiweza,” alisema Omary.
Hata hivyo, aliomba wizara
husika kuharakisha upatikanaji wa hati ya kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa kituo
cha kisasa cha kutolea misaada (Center) cha Pugu.
“Uwepo wa Msama katika
ulimwengu huu kunamuwakilisha Mwenyezi Mungu, kwani Mungu si mbaguzi kwa watu
wake, anawapenda wote na anatoa sawa kwa kila mtu, hivyo ndivyo alivyo Msama,
kwa moyo mmoja namuombea yeye na taasisi yake isiyokuwa na ubaguzi wa dini
kuendelea kuwa hivyo wakati wote,” alisema Omari.
No comments:
Post a Comment