HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 04, 2013

RAIS TFF AUNDA KAMATI MBILI MAALUMU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda kamati mbili maalumu (ad hoc) kwa ajili ya kutathmini muundo wa ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha, na kutahmini muundo wa Bodi ya Ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha ikiwemo kuunda kampuni.

Kamati ya Kutathmini Muundo wa Ligi inaongozwa na Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla wakati Katibu ni Ofisa Mashindano wa TFF, Idd Mshangama. Wajumbe ni Rahim Kangezi, Amri Said, Sunday Manara, Salim Bawazir na Lucas Kisasa.

David Nchimbi kutoka Delloitte ndiye anayeongoza Kamati ya Muundo wa Bodi ya Ligi wakati wajumbe ni Edwin Kidifu (Mwanasheria wa SUMATRA), Jones Paul (Mkurugenzi wa Sunderland/Symbion Academy), Evans Aveva, John Jambele, Masoud Sanani na Pelegrinius Rutahyuga.

Wakati huo huo, Rais Malinzi amemteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa Mshauri wa Rais (Ufundi). Mshauri wa Rais (Utawala) atateuliwa baadaye.

TIKETI 260 KOMBE LA DUNIA BRAZIL
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeipa Tanzania mgawo wa tiketi 260 za Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.

Watanzania wanaohitaji tiketi hizo wanatakiwa kutuma maombi TFF kwa maandishi wakielezea aina ya tiketi na mechi wanazotaka kushuhudia. Hakuna tiketi zitakazoombwa FIFA bila kuwepo maombi kwa maandishi.

Tiketi zilizopo kwa Tanzania ni ifuatavyo; kwa hatua ya makundi (ukiondoa mechi ya ufunguzi), raundi ya 16 bora, robo fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ni 250.

Kwa mechi ya ufunguzi, nusu fainali mbili na fainali (mechi namba 1, 61, 52 na 64) ni tiketi kumi tu ndizo zitakazopatikana. Bei za tiketi ziko katika viwango vitatu tofauti.

Mechi ya ufunguzi tiketi zake ni dola za Marekani 495, 330 na 220. Hatua ya makundi (mechi namba 2-48) ni dola 175, 135 na 90. Hatua ya 16 bora (mechi namba 49-56) ni dola 220, 165 na 110.

Robo fainali (mechi namba 57-60) ni dola 330, 220 na 165 wakati nusu fainali (mechi namba 61 na 62) ni dola 660, 440 na 275. Mechi ya mshindi wa tatu ni dola 330, 220 na 165. Kiingilio kwa fainali kitakuwa dola 990, 660 na 440.

TFF itawasilisha maombi ya tiketi hizo FIFA kuanzia Desemba 8 mwaka huu  hadi Februari 7 mwakani. Idadi ambayo itaombwa FIFA itatokana na Watanzania waliowasilisha maombi TFF kwa vile zinaweza zisipatikane tiketi zote hizo zilitengwa kwa Tanzania.

Hivyo tunasisitiza maombi ya tiketi yatakayofanyiwa kazi ni yale ambayo yamewasilishwa TFF kwa maandishi tu.

AFRIKA KUSINI KUTUA KWA SOUTH AFRICA AIRWAYS
Kikosi cha Afrika Kusini (Basetsana) kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Tanzania (Tanzanite) kinatua nchini kesho (Desemba 5 mwaka huu).

Afrika Kusini itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) itatua saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South Africa Airways.

Wanaounda Basetsana ni makipa Kaylin Swart, Regirl Ngobeni na Juliet Sethole. Mabeki ni Abongile Dlani, Caryn van Reyneveld, Chamelle Wiltshire, Meagan Newman, Nomonde Nomthseke, Tiisetso Makhubela na Vuyo Mkhabela.

Viungo wapo Amanda November, Amogelang Motau, Gabriella Salgado, Koketso Mamabolo, Nomvula Kgoale na Thembi Kgatlane. Washambuliaji ni Mosili Makhoali, obyn Moodaly, Sduduzo Dlamini na Shiwe Nogwanya.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na orange, sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa sh. 10,000.

JOPO LA WATAALAMU KUPANGA MKAKATI WA AFCON 2015
Jopo la wataalamu 20 walioteuliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi linakutana kupanga mkakati wa kuonesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2015 nchini Morocco.

Kikao hicho maalumu (retreat) kitafanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6-8 mwaka huu. Jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Omari Kipingu.

Wengine wanaounda jopo hilo linalohusisha pia makocha ni Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah Kibaden, Pelegrinius Rutahyuga, Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Boniface Mkwasa, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso.

Wajumbe wengine wa jopo hilo wanatoka Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages