HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 03, 2014

LINDI SOCCER ACADEMY (LSA) WATEMBELEA OFISI ZA TANZANIA DAIMA
 Kiungo-mshambuliaji wa Lindi Soccer Academy (LSA), Hamdani Sarahani akimkabidhi Mhariri wa Habari wa gazeti la Tanzania Daima, Martin Marela, Kombe la Ubingwa wa Chama cha Soka Manispaa ya Lindi (LIMFA CUP 2013). LSA walitembelea Ofisi za Tanzania Daima leo kutoa shukrani kwa sapoti inayopewa na gazeti hilo kwa ustawi wa kituo na timu zake za vijana. 
 Mwandishi Mwandamizi wa Michezo wa Tanzania Daima, Clezencia Tryphone (wa pili kushoto), akiwaeleza jambo wachezaji wa LSA walipotembelea Idara ya Matangazo ya gazeti hilo leo mchana. Wa kwanza kushoto ni Meneja Matangazo, Twalib Mungulu.
 Kiungo-mshambuliaji wa Lindi Soccer Academy (LSA), Hamdani Sarahani akimkabidhi Meneja Usambazaji Msaidizi wa gazeti la Tanzania Daima, Antidius Karumuna, Kombe la Ubingwa wa Chama cha Soka Manispaa ya Lindi (LIMFA CUP 2013), walipotembelea Idara ya Uzalishaji na Usambazaji.
 Mhariri wa Tanzania Daima Jumatano, Edson Kamukara, akipokea Kombe la Ubingwa wa Chama cha Soka Manispaa ya Lindi (LIMFA CUP 2013) kutoka kwa mchezaji wa LSA, wakati kikosi hicho kilipotembelea Chumba cha Habari cha gazeti hilo leo.
 Mhariri wa Habari wa Tanzania Daima, Martin Marela, akizungumza na wachezaji wa LSA walipotembelea Chumba cha Habari cha gazeti hilo leo mchana.
 Mhariri wa Michezo na Burudani wa Tanzania Daima, Tullo Chambo (wa tatu kulia), akizungumza na wachezaji wa LSA walipotembelea Chumba cha Habari leo mchana wakiwa safarini kutoka Zanzibar walikokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Muungano kwa Vijana chini ya miaka 14 kurejea Lindi.
Mkurugenzi wa LSA, Haffidh Karongo, akitoa shukrani wakati alipowaongoza wachezaji wa timu hiyo kutembelea Chumba cha Habari cha Tanzania Daima leo mchana.

DAR ES SALAAM, Tanzania

LSA wako Dar es Salaam kwa siku kadhaa, wakiwa safarini kurejea Lindi kutokea Zanzibar, walikokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Muungano kwa vijana chini ya miaka 14, ambako waliishia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya kila mwaka

MSAFARA wa wachezaji 20 wa Lindi Soccer Academy (LSA), ya mjini Lindi, leo umetembelea Ofisi za Kampuni ya Free Media Ltd wachapishaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari na kutoa shukrani kwa sapoti wanayopewa na magazeti hayo.

Akizungumza wakati wa kutoa neno la shukrani wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa LSA, Haffidh Karongo, aliishukuru Free Media, kwa magazeti yake kuwa kinara wa vyombo vya habari nchini, vyenye mchango mkubwa katika ustawi wa kituo chake.

“Kwa niaba ya wazazi, walezi, wadau na wachezaji wa LSA, napenda kufikisha kwenu salamu za shukrani, kwa mchango uliotukuka, ambao umekuwa chachu ya mafanikio ya kituo hiki ndani na nje ya uwanja,” alisema Karongo.

Aliongeza kuwa, harakati chanya za kituo katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wa umri tofauti wa kituo hiko zinakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini kupitia mchango wa Tanzania Daima na Sayari, wameweza kuzikabili na kusonga mbele.

Karongo aliyataka magazeti hayo kutoishia hapo, badala yake wajikite zaidi katika kuwawezesha kusaidia misaada mbalimbali na wadau wa soka nchini, ikiwamo mialiko ya kushiriki michuano mbalimbali kwa maendeleo ya vipaji vya vijana.

Wachezaji hao ambao walikiri kufurahishwa na ziara yao hiyo ya pili katika kipindi cha miaka mitatu, walitembelea Idara ya Matangazo, Uzalishaji na Usambazaji na Chumba cha Habari, ambako walijifunza hatua mbalimbali za utayarishaji wa magazeti hayo.

LSA wako Dar es Salaam kwa siku kadhaa, wakiwa safarini kurejea Lindi kutokea Zanzibar, walikokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Muungano kwa vijana chini ya miaka 14, ambako waliishia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

Pages