Dar es Salaam, Tanzania
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo mmoja inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja.
Timu itakayoongoza katika kila kituo cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2 mwaka huu ndiyo itakayopata tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu ujao wa 2014/2015. Vituo hivyo ni Mbeya, Morogoro na Shinyanga.
Kituo cha Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu za Abajalo FC ya Dar es Salaam, African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Mji Mkuu FC (Dodoma) Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja wa Sokoine ndiyo utakaotumika katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC ya Arusha, Magereza FC (Iringa), Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji FC (Njombe), Panone FC (Kilimanjaro), Tanzanite SC (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro).
Timu za Eleven Stars ya Kagera, Geita Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC (Mara), Mbao FC (Mwanza), Milambo SC (Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma), Simiyu United (Simiyu), Singida United (Singida) na Wenda FC (Mbeya) zitacheza katika kituo cha Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage.
Orodha ya usajili wa wachezaji wa timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi ambacho kinamalizika Mei 4 mwaka huu.
Hata hivyo, katika usajili uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa kuna wachezaji walioshiriki VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi msimu wa 2013/2014.
Kiongozi yeyote atakayebainika katika udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa klabu au chama cha mpira wa miguu cha mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya kimaadili vya TFF kwa hatua zaidi.
Ligi ya Mabingwa haina mdhamini, hivyo timu shiriki zitajitegemea kwa kila kitu, na zinakumbushwa kuwahi vituoni.
MALAWI KUWASILI MEI 1 KUIVAA STARS
Timu ya Taifa ya Malawi (Flames) inatarajiwa kuwasili nchini Mei 1 mwaka huu kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Mei 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Flames yenye msafara wa 31 utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Malawi (FAM) utaingia Mbeya kwa usafiri wa barabara. Wachezaji katika msafara huo ni 20.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha mpya, Mart Nooij tayari ipo jijini Mbeya kujiwinda kwa mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment