Na Hillary Shoo, Singida
WATU 19 wamekufa, wakiwemo askari polisi wanne na wengine nane kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea ajali mbaya ya kugongwa na basi la abiria katika eneo la kijiji cha Utaho Kata ya Puma Wilayani Ikungi , Barabara Kuu ya Singida- Dodoma umbali ya kilomita 15 kutoka Singida Mjini.
Ajali hiyo imetokea juzi majira ya saa 2.45 usiku na kulihusisha basi lenye namba za usajili T 799 BET aina ya Nissan mali ya Kampuni ya Sumry, likitokea Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa polisi Mkoani Singida (SACP), Geofrey Kamwela alisema siku ya tukio hilo wananchi pamoja na askari polisi waliokuwa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara, wakujiandaa kuupakia mwili ya mwananchi mmoja mwendesha baiskeli aliyegongwa na lori katika eneo hilo na kufariki dunia.
Alisema walikuwa katika harakati za kuupakia mwili wa marehemu ndani ya gari la polisi PT 1424 likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara.
Kamanda Kamwela alisema,gafla basi hilo liliwagonga watembelea kwa miguu hao na kusababisha vifo vya watu 15 papo hapo huku wengine, watatu wakifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu.
Hata hivyo alisema dereva wa basi hilo aitwae Paul Njilo mkazi wa jijijini Dar es Salaam, alipokaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limepaki pembeni kushoto mwa barabara na askari pamoja na wananchi wa eneo hilo, lakini katika nia ya kulikwepa gari la polisi,ndipo alipovamia kundi hilo la watu pamoja na askari na kuwagonga.
Aidha alisema dereva wa basi hilo baada ya kufanya ajali hiyo hakusimama na kwenda kulitelekeza basi eneo la Ikungi zaidi ya kiliomita 25 kutoka eneo la tukio na kisha kukimbia kusikojilikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Aliwataja askari waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida.
Pia aliwataja wengine waliokufa kuwa ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Utaho Ramadhan Mjengi, Paul Hamis Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho, Ernet Salanga mwenyekiti Kitongoji cha Utaho,Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan Mwinyi Hamis, na Issa Hussein wote wakazi wa kijiji cha Utaho.
Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na huku taratibu za kitabibu zikiendelea na imehifadhiwa katika chumba cha maiti hospitali ya mkoa wa singida.
Majeruhi wawili wamelazwa katika hospitali ya Mkoa na wengine sita katika hospitali ya misioni ya Malkia wa Ulimwengu Puma.
Aidha miili ya askari polisi inatarajiwa kusafirishwa kwenda mikoani wanakotoka wakati wowote mara taratibu za kipolisi zikikamilika ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ndugu zao wa Rombo, Pwani, Mablizi Mbeya na Iringa.
Akizungumzia juu ya ajali hiyo Kamanda Kamwela alisema awali majira ya sa 1:30 usiku ilitokea ajali ya mtembea kwa miguu Gerad Zefania aliyegongwa na lori na kufa papo hapo.
Uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na kumtafuta dereva wa basi la Sumry ili aweze kuhojiwa na kasha hatua za kisheria zeweze kuchukuliwa dhidi yake.
No comments:
Post a Comment