Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu wakitoa msaada wa huduma ya kwanza kwa mfanyakazi wa Ikulu, Rashid John Chilwangwe (45), ambaye alidondoka na kupoteza fahamu wakati wa Maadhimishisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Hata hivyo baadae aliripotiwa kufariki dunia. (Picha na Francis Dande)
Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu wakitoa msaada kwa Rashid John Chilwangwe mara bada ya kuanguka.
Mwili wa marehemu Rashid John Chilwangwe ukiwekwa katika gari la wagonjwa kwa ajili ya kwenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Temeke.
Na Shabani Matutu na Shehe Semtawa
MAADHIMISHO ya sherehe za Siku
ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Uhuru
jijini Dar es Salaam jana, yameingia dosari baada ya ofisa wa Ikulu, Rashid
John Chilwangwe kufariki dunia akiwa katika maadhimisho hayo.
Chilwangwe alipatwa na tukio
hilo majira ya saa nne asubuhi, nje ya Uwanja wa Uhuru akiwa anasubiri kuingia
na maandamano yaliyokuwa yakipita uwanjani mbele ya Rais Jakaya Kikwete,
yakitokea viwanja vya Mnazi Mmoja.
Walioshuhudia tukio hilo,
wasema kuwa kuwa Chilwangwe ambaye anafanya kazi katika moja ya
idara za Ikulu jijini Dar es Salaam, alianguka ghafla na kisha kubebwa na
wafanyafakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na kuhifadhiwa kwenye moja ya
mahema yaliyoandaliwa uwanjani hapo kwa ajli ya huduma za dharura.
Akiwa ndani ya hema hilo,
baadhi ya madaktari walijitahidi kutoa huduma ya kwanza ya matibabu, lakini
hata hivyo alifariki dunia wakati akiendelea kupata matibabu.
Haikuweza kujulikana sababu
hasa ya kifo cha ofisa huyo wa Ikulu kwani madaktari waliokuwapo eneo hilo
hawakuwa tayari kuzungumzia kwa kina tukio hilo la kusikitisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Englibert Kiondo,
alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema limetokana na Chilwangwe
kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kisukari.
Kiondo alisema kuwa kifo hicho
kilichangiwa na mwendo mrefu aliotembea na kusababisha kuamsha maradhi yake ya moyo
na kisukari, na hivyo kupoteza nguvu na kuanguka ghafla hatimaye kupoteza
maisha.
Kiondo alisema kuwa baada ya
kufariki, mwili wake ulipelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa
uchunguzi zaidi.
Mbali na tukio hilo, watu tisa wakiishiwa nguvu wakiwa uwanjani na kuanguka
kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Mganga mmoja wa Manispa ya Temeke aliyegoma kutaja jina lake, aliyekuwa
akiwahudumia wagonjwa hao katika hospitali ya uwanjani hapo, alisema chanzo cha
kuanguka kimetokana na baadhi yao kufika
uwanjani hapo bila kula.
Mganga huyo alifafanua kuwa
wapo watu wanne ambao walianguka kutokana na ukosefu wa sukari mwilini.
Alisema watu watatu
waligundulika kuwa na shinikizo la damu huku wengine wawili wakisumbuliwa na
malaria, hata hivyo watu hao walipatiwa tiba na kuruhusiwa kurudi majumbani
kwao.
No comments:
Post a Comment