Na Lucy Ngowi
KATIBU wa Mawasiliano Jimbo la Misheni Mashariki katika
kanisa la Moravian, Emaus Mwamakula ameshauri kuwepo na suluhu miongoni mwa
pande mbili za kanisa hilo zilizopo kwenye mgogoro.
Mwamakula alitoa ushauri huo katika ibada ya Jumapili
iliyofanyika chini ya mti, jirani na Kanisa la Morovian, Kinondoni baada ya
upande mmoja wa mgogoro kuwazuia upande wa pili wasiabudu katika kanisa hilo.
Alisisitiza kuwa, mpaka sasa katika pande hizo mbili hakuna
mwenye haki hata mmoja mpaka pale suluhu itakapopatikana, ambapo uongozi wa juu
duniani umetoa miezi sita ili upatikane ufumbuzi, hapo ndipo tamko la mwisho
litakapotolewa.
“Waumini hawa wamekubaliana wasali chini ya mti kuepusha
vurugu. Viongozi wetu wameruhusu usuluhishi uendelee na katika kipindi hichi
cha mgogoro kila upande uzingatie amani,” alisema Mwamakula.
Aliongeza kuwa, “ Mungu wetu ni wa haki. Yeyote ambaye
anaadhili fujo, huyo Mungu atashughulika n aye na yeyote Yule anayepokea fedha
kwa jinsi yoyote ile ili mgogoro huo usimalizike Mungu atashughulika naye,”
alisema.
Waumini hao waliosalia chini ya mti, awali walikuwa wakisali
katika jingo la kanisa hilo ghorofani na wale ambao wana mgogoro nao walikuwa
wakisali jengo hilo hilo chini, lakini milango yao imefungwa hali iliyowafanya
washindwe kusali katika jengo hilo.
Kwa upande wake Mchungaji Sauli Kajula ambaye ndiye mwenye
washirika waliobaki kwenye jingo hilo, alisema kuwa, wamechukua hatua ya
kufunga milango ya juu kwa huo upande wa pili wa mgogoro kwa kuwa wameona kuwa
wanavurugu.
Alisisitiza kuwa, hata wao wanapenda kupata suluhu la jambo
hilo kwa kukaa meza moja na upande wapili wanaopingana nao.
Baadhi ya majirani wanaozunguka eneo hilo la kanisa,
walikiri kuwepo kwa mgogoro huo ambao umekuwa ukiwakosesha raha, hivyo wameomba
pande hizo mbili zipatane.
Wakiomba wahifadhiwe majina yao, walikiri kuwa upande mmoja
unatumiwa na mfanyabiashara mwenye fedha hali inayofanya mgogoro huo ushindwe
kupata suluhu.
Siku za karibuni kulikuwa na mkutano mkuu wa viongozi wa juu
wa kanisa hilo duniani, ambao walitoa miezi sita suala hilo liwe limekwisha,
baada ya hapa watatoa tamko nini kafanyike.
No comments:
Post a Comment