HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2014

Ni mtikisiko wa nyimbo za Injili Shinyanga, Mwanza

Malope, Muhando, Sarah K kuwashika Kambarage, CCM Kirumba
.Wakazi Kanda ya Ziwa kujionea kivumbi Jumamosi na Jumapili

Na Mwandishi Wetu
Malope

MALIKIA wa Muziki wa Injili Afrika, Rebecca Malope wa Afrika Kusini, yu miongoni mwa waimbaji kutoka nje ya Tanzania ambao Jumapili ya Mei 4, watakuwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kutoa burudani ya nguvu kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa nyimbo za injili.   Kwake ni mara ya pili kuja nchini kwa mwaliko wa Kampuni ya Msama Promotions Ltd ya jijini Dar es Salaam kwani mara ya kwanza ilikuwa Aprili 6, 2012.

Nguli huyu wa muziki wa ijili, amekuja kwa mwaliko wa Kampuni hiyo inayoasisi tamasha la Pasaka ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka tangu mwaka 2000 pamoja na Tamasha la Krismas lililofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2013.

Kutokana na umahiri mkubwa ambao alionesha mwanamama huyo katika tamaska la mwaka 2012 katika Uwanja wa 
Taifa, jijini Dar es Salaam mbele ya aliyekuwa mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, ndio maana amealikwa kwa mara nyingine.

Kwa mujibu wa Alex Msama ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu Tamasha hilo la Pasaka na Mkurugenzi
wa Msama Promotions, Malope anajisikia faraja kuja nchini kwa mara nyingine akisema anaipenda Tanzania na watu wake waliojaa ukarimu.

Anasema, ujio wa Malope ni kutokana na maombi ya wapenzi na mashabiki wengi, hivyo kamati yake ikaona wamlete kwa heshima yao katika harakati zao za kuendelea kulipa hadhi na heshima inayostahili tamasha hilo la kimataifa.

Msama anasema, Malope anatarajiwa kutua jijini Dar es Salaa leo kabla kesho kusafiri hadi jijini Mwanza kwa Tamasha litakalofanyika Jumapili katika Uwanja wa Kirumba na kuongeza kwamba maandalizi yameshakamilika.

“Baaada ya Malope kutua jijini Dar es Salaam leo (leo), atasafiri hadi jijini Mwanza kwa onesho la Muziki wa Injili ikiwa ni mwendelezo wa kishindo cha Tamasha la Pasaka ambalo lilizinduliwa April 20 katika Uwanja wa Taifa na Waziri Membe (Benard),” anasema.

Msama anasema, baada ya uhondo wa tamsha hilo kufanyika Uwanja wa Taifa (Aprili 20) na Uwanja wa Jamhuri, Morogoro (April 21), ni zamu ya Kanda ya Ziwa, ukianzia Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga hapo kesho kabla ya Jumapili kutikisa katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Anatoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi kuzoa baraka za Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo kutoka kwa waimbaji mahiri wakiongozwa na Malope ambaye ameahidi kufanya vitu vya uhakika katika kuutangaza utukufu wa Mungu.

Msama anasema mbali ya Malope, waimbaji wengine ambao watapamba tamasha hilo kutoka nje ni Ephraem Sekereti kutoka Zambia na Sarah Kiarie wa Kenya ambao watakuwa smabamba na waimbaji mahiri wazawa wakiongozwa na malikia wa Muziki wa injili Tanzania, Rose Muhando.

“Niwasihi tu wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili wa Kanda ya Ziwa kwamba, sasa ni zamu yao kupata baraka za Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo kutoka kwa waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania, wasikose kufika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga (Jumamosi) na Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza (Jumapili),” anasema.

Anasema kwa maandalizi yaliyofanywa na waimbaji wote pamoja na kamati yake, ni matarajio yake litakuwa ni tamasha litakaloacha simulizi sio tu mkoani Shinyanga na Mwanza, bali katika Kanda ya Ziwa na vitongoji vyake.

Kuhusu maudhui, Msama anasema mbali ya lengo la msingi ambalo ni kueneza ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya uimbaji, pia Kamati yake itaendelea kutumia sehemu ya mapato kusaidia makundi maalumu katika jamii wakiwamo yatima, walemavu na wajane.

Anasema zaidi ya hapo, tamasha la mwaka huu litaendeklea kuhimiza amani na upendo kama ilivyo kawaida yake tangu kuasisiwa kwake ambapo kwa mwaka huu linabebwa na kauli mbiu ya ‘Uzalendo Kwanza, Haki Huinua Taifa’.

Msama anasema uliangalia kwa undani Tamasha la Pasaka, ni kielelezo cha upendo na amani kwani limekuwa likiwaleta pamoja watanzania bila kujali tofauti za dini zao, itikadi, kabila wala jinzia, hivyo walichofanya mwaka huu ni kuongeza tu msisitizo.

Anasema nje ya maudhui hayo kuntu, kwa upande wake analitumia tamasha la mwaka huu kumshukuru Mungu kumwepusha na kifo katika ajali mbaya ya gari iliyotokea April 11, katika eneo la Ipagala, nje kidogo ya mji wa Dodoma, akitokea jijini Dar es Salaam.

Msama anasema licha ya gari aliyokuwa akiendesha kupinduka mara tatu, hana budi kumshukuru Mungu, yu mzima wa afya  kwani licha ya kupata maumuvu ya kifua na bega la kulia, baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Dodona na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam.

Anawasihi wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, kujitoikeza kwa wingi katika maonesho yote mawili katika Uwanja wa Kambarage na CCM Kirumba, kujionea umahiri wa waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania ambao kwa uweza wa Mungu, wamejipanga kuangusha burudani ya nguvu.

No comments:

Post a Comment

Pages