Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania
(TanTrade), Jacqueline Mneney Maleko, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Utamaduni Duniani na Uhuru wa Afrika
yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia tarehe 20-25 yenye kauli
mbiu ya “Tudumishe Amani Yetu, Tuuenzi Utamaduni Weu’. Kushoto ni Mratibu
wa Taasisi ya Tan Tanzania, Deusdedit Kizito. (Na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo pamoja na TAN-TANZANIA wameandaa Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Utamaduni Duniani na Uhuru wa Afrika yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia tarehe 20 mpaka 25 Mei, 2014 yenye Kauli Mbiu ya “TUDUMISHE AMANI YETU, TUUENZI UTAMADUNI WETU”.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bi. Jacqueline Mneney Maleko, amesema Maonesho haya yanatarajia kushirikisha Wajasiriamali wapatao 150 kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 21 Mei 2014 na Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo.
Amesema, Maonesho haya yanakwenda sambamba na Sherehe za Siku ya Utamaduni Duniani (tarehe 21 Mei, 2014) na Siku ya Afrika (tarehe 25 Mei, 2014). Wageni mbalimbali toka ndani na nje ya nchi wamepewa mwaliko wa kutembelea Maonesho haya.
Akizungumzia chimbuko la Maonesho haya, Bibi Maleko amesema, huu ni Mpango Mkakati wa TanTrade wa kukuza na kuendeleza huduma na bidhaa asili za Tanzania ambazo zina uwezo wa kupata fursa za masoko hivyo kuchangia katika kukuza kipato kwa wadau na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amesema TanTrade inalenga kuamsha hamasa ya kununua bidhaa na huduma za Tanzania hususani za jadi ambazo kwa kiasi kikubwa hazina ushindani. Kama moja ya utekelezaji wa mkakati huu,
Bibi Maleko, anasema TANTRADE imeandaa maonyeswho haya maalum, kuguatia mafanikio yaliyopatikana katika Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar-es-Salaam Mwaka 2013, ambapo TanTrade iliandaa Banda Maalum la Tanzania lililokuwa na Eneo maalum la bidhaa za ya sanaa na utamaduni.
Bibi Maleko, amesisitiza lengo la Maonesho haya ni kuwezesha Wadau mbalimbali wa Tasnia ya Sanaa na Utamaduni wakiwemo Wachongaji, Washonaji, Wafinyanzi, Wasindikaji na Wasanii wakiwemo wasanii wa filamu, kuonesha bidhaa na sanaa zao kwa nia ya kupata masoko ya ndani pamoja na yale ya nje ya nchi.
Bibi Maleko amesema Maonesho haya yatakwenda Sambamba na michezo ya jadi, ngoma za utamaduni, muziki na vionjo vya vyakula vya Kitanzania kuwezesha watembeleaji wa Maonesho kupata burudani na ladha ya vyakula vya makabila mbalimbali yaliyopo hapa nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa Taasisi ya Tan Tanzania, Deusdedit Kizito amesema taasisi yake imekuwa ikiratibu siku Afrika kwa miaka mitano mfulululizo, hivyo sasa kwa kushirikiana na TANTRADE na Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, wameunganisha na maadhimisho ya siku ya Utamaduni na kuandaa maonyesho hayo kwa pamoja!.
Bw. Kizito amesema Wananchi wa watapata fursa ya kusherekea siku ya Afrika kwa kukuza masoko ya bidhaa zao huku wakikuza Utamaduni na Sanaa ya Tanzania ili bidhaa na huduma hizo ziweze kupata soko la ndani na nje ya Nchi.
Maonyesho hayo ni fursa ya kuamsha hamasa ya kupenda bidhaa na sanaa za Tanzania na wakati huo huo kuwaunganisha Wadau wa Tasnia za sanaa na utamaduni kukaa pamoja, kushirikiana hivyo kuimarisha Taasisi zao na kuhamasisha maudhui ya “Sanaa ni Uchumi” ambapo wananchi wengi wanatarajiwa kuhamasishwa kushiriki katika shughuli za Sanaa kwa nia ya kuongeza kipato chao na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment