Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la
Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija (kushoto) akikabidhi hundi yenye thamani ya
shilingi milioni 15 kwa Paroko Msaidizi wa Kigango cha kanisa la Mavurunza, Padri Xavery
Kassase (kulia) kusaidia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mapadri wakati wa
harambee iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa la Mtakatifu Rita hivi
karibuni.
Paroko Msaidizi wa Kigango cha Kanisa la Mavurunza,
Padri Xavery Kassase(kulia) akionyesha hundi ya shilingi milioni 15
zilizotolewa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa kigango
cha Kanisa la Mtakatifu Rita jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mchango huo wa
kampuni ulitolewa kusaidia ujenzi wa nyumba ya mapadri kanisani hapo. Kushoto
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija.
Na Mwandishi Wetu
MAENDELEO ya kijamii na kiuchumi yataweza kupatikana endapo tu kila mtu ataweza kutoa mchango wake kuwasaidia wale wanaohitaji msaada ili kubadilisha maisha yao na kuwa wachangiaji wakubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw. Simon Bulenganija
wakati wa harambee ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya mapadri katika Kigango cha
kanisa la Mtakatifu Rita lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, ambapo UDA
ilichangia shilingi milioni 15.
“Watanzania wasisubiri mpaka
makampuni makubwa yajitokeze na kutusaidia kubadilisha hali zetu za kiuchumi na
mfumo wetu wa maisha. Mabadiliko yataweza kufikiwa tu endapo kila mmoja wetu
ataweza kuchangia kwa nafasi yake kikamilifu. Makampuni yote makubwa na madogo
na watu binafsi wenye uwezo wa kusaidia, wawashike mkono wale wanaohitaji
msaada ili tuweze kuendelea pamoja,” alisema.
Bw. Simon Bulenganija alisema kuwa
kampuni yake imekuwa ikijihusisha na shughuli mbali mbali za kijamii ikiwa ni
jitihada madhubuti zinazolenga katika upatikanaji wa maendeleo miongoni mwa
watanzania wote.
Alisema kuwa shilingi milioni 15
zilizotolewa na UDA zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupiga jeki maendeleo ya
kanisa hilo hususani katika ujenzi wa nyumba ya mapadri na baadae kuendelea na
mradi wa ujenzi wa kanisa jipya.
“Japokuwa bado kampuni yetu ni
kampuni changa ya kitanzania, tumeunda programu yetu ya shughuli za kijamii
katika namna ya kwamba shughuli tunazojihusisha nazo, zitasaidia katika
kutekeleza ajenda yetu yenye kaulimbiu “ukuaji wa kampuni yetu uwe sambamba na
ukuaji wa kiuchumi wa jamii yetu”. Hii pia ni njia pekee ya kurudisha sehemu ya
pato letu kwa jamii,” alisema Bw. Bulenganija.
Naye, Bw. Frederick Msumali,
Mwenyekiti wa Kigango cha Mtakatifu Rita, aliipongeza kampuni hiyo kwa mchango
wake na ushiriki wa Mkurugenzi wa UDA wakati wa shughuli hiyo ya harambee
ambayo iliwezesha kanisa hilo kukusanya zaidi ya shilingi milioni 60
zitakazotumika katika mradi huo.
“Tungependa kwa kiasi kikubwa kutoa
shukrani zetu kwa mchango uliotolewa na UDA. Msaada huu
kwa kiasi kikubwa utasaidia kupiga jeki mradi wetu wa ujenzi wa nyumba ya
mapadri na baadae kuendelea na ujenzi wa kanisa jipya utakaofanyika karibu na
kanisa hili la sasa.
“Lakini pia, tunaishukuru UDA kama
kampuni na Bw. Bulenganija mwenyewe kwa kuwa mgeni wetu rasmi. Mfano huu
unahitaji kuigwa na makampuni mengine nchini,” alisema Bw. Msumali.
No comments:
Post a Comment