HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 05, 2026

IMBEJU NDONDO CUP 2026 KUJA KIVINGINE, CRDB YATOA MILIONI 400

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule (kulia), akicheza ngoma ya kikundi cha uhamasishaji wakati wa uzinduzi wa Imbeju Ndondo Cup Jiongezee yaliofanyika jijini Dar es Salam.


Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa (katikati), 
akicheza ngoma ya kikundi cha uhamasishaji wakati wa uzinduzi wa Imbeju Ndondo Cup Jiongezee yaliofanyika jijini Dar es Salam.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


DAR ES SALAAM – Katika jitihada za kuendeleza na kuboresha mashindano ya Imbeju Ndondo Cup msimu wa 13 mwaka 2026, Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation imetenga jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo pamoja na zawadi mbalimbali kwa washiriki.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwamba, alisema kuwa msimu huu wa Imbeju Ndondo Cup utakuwa wa kipekee kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa lengo la kuongeza ushiriki wa vijana na kuinua hadhi ya mashindano hayo kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa.



“Msimu huu wa Imbeju Ndondo Cup 2026 tumekuja na maboresho makubwa zaidi. Tumelenga kuongeza fursa za ushiriki na kuboresha mashindano ili yawe makubwa zaidi na yenye ushindani wa hali ya juu kuanzia mashinani hadi ngazi ya mkoa,” alisema Tully.

Alieleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya zawadi, ambapo bingwa wa mashindano hayo atajishindia shilingi milioni 30 pamoja na timu yake kulipiwa gharama za kuhudhuria mechi moja ya AFCON itakayochezwa jijini Dar es Salaam. Mshindi wa pili ataondoka na kitita cha shilingi milioni 20.

Aidha, alisema kuwa zawadi mbalimbali zitatolewa kwa timu zitakazofuzu katika hatua tofauti za mashindano hayo. Kwa upande wa tuzo binafsi, mchezaji bora atapata shilingi milioni 3, huku mfungaji bora, kipa bora na beki bora kila mmoja akizawadiwa shilingi milioni 1.



Tully aliongeza kuwa waandaaji wamewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha hadhi ya kombe na medali za mashindano hayo ili viwe katika viwango vya kimataifa.

“Tunalenga kuifanya ligi hii kuwa kubwa zaidi na yenye heshima. Kombe pamoja na medali zake vinatengenezwa kwa viwango vya kimataifa, na kwa sasa kuna timu maalumu imekwenda China kwa ajili ya kutengeneza vifaa hivyo. Tutavizindua rasmi pindi vitakapokamilika,” alisema.



Kwa upande wake, mtangazaji wa michezo Shafii Dauda aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha vijana kupitia michezo na elimu.

“CRDB imekuwa mshirika wetu wa muda mrefu na imefanya kazi kubwa ya kuwainua vijana. Mara nyingi changamoto si kwamba watu hawataki kufanya mambo makubwa, bali hawapati fursa au mwongozo sahihi wa kuwawezesha kufikia malengo yao,” alisema Shafii.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, aliisifu Benki ya CRDB kwa ubunifu wake katika utoaji wa huduma na namna inavyowafikia makundi mbalimbali ya wananchi.

Mtambule pia aliwahakikishia wadau wa soka kuwa suala la usalama wakati wote wa mashindano hayo limepewa kipaumbele, akisema kuwa ulinzi utaimarishwa ndani na nje ya viwanja vitakavyotumika.

“Jeshi la Polisi pamoja na Polisi Kata katika maeneo husika watashirikishwa kikamilifu kuhakikisha usalama na utulivu vinadumishwa wakati wote wa mashindano,” alisema Mtambule.


No comments:

Post a Comment

Pages