Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB imefunga rasmi kampeni ya “Fainali Ndo Mpango na TemboCard Visa”, huku washindi mbalimbali wakijinyakulia zawadi zikiwemo safari za kwenda kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia nchini Canada na Marekani pamoja na televisheni kubwa za kisasa za inchi 85.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi wa CRDB, Karington Chahe, alisema kampeni hiyo ilianza Februari 12, 2026 na imehitimishwa rasmi leo baada ya kuendeshwa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Chahe alisema jumla ya washindi 20 wamepatikana kupitia kampeni hiyo. Kati yao, washindi 10 watapata fursa ya kwenda kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia, ambapo sita watasafiri kwenda Canada na wanne kwenda Marekani.
Alifafanua kuwa washindi hao watagharamiwa gharama zote za safari na malazi na Benki ya CRDB ili waweze kushuhudia kwa karibu michuano hiyo ya kimataifa.
Mbali na safari hizo, washindi wengine 10 wamejishindia televisheni kubwa za kisasa za inchi 85 pamoja na ving’amuzi, ikiwa ni sehemu ya motisha kwa wateja wanaotumia huduma za TemboCard Visa.
Aidha, Chahe aliwashukuru Watanzania na wateja wa Benki ya CRDB kwa kuendelea kutumia huduma za benki hiyo na kuunga mkono matumizi ya malipo ya kidijitali, akisisitiza kuwa kampeni hiyo imelenga kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya malipo nchini.
Alisema benki hiyo itaendelea kubuni kampeni mbalimbali zitakazoongeza thamani kwa wateja wake na kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.




No comments:
Post a Comment