Kampuni ya kuzalisha bidhaa za watoto na akina mama, Bumpietz, imetoa ufadhili wa mwaka mmoja kwa mama aliyejifungua mapacha watano, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha mshikamano na kusaidia familia zinazokabili changamoto za malezi ya watoto wachanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya Bumpietz, Lwiza Fulgence, alisema kuwa kampuni hiyo imeguswa na tukio hilo la kipekee na kuamua kujitokeza kutoa msaada utakaomsaidia mama huyo katika kuwalea watoto wake.
Lwiza alisema kuwa kujifungua watoto watano kwa wakati mmoja ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa na matumizi ya kila siku ya bidhaa mbalimbali za watoto, hali ambayo inaweza kuwa mzigo mkubwa kwa familia husika.
Kutokana na hali hiyo, Bumpietz imeona umuhimu wa kushiriki jukumu la kijamii kwa kutoa bidhaa muhimu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Tumeguswa sana na tukio hili. Kama wazalishaji wa bidhaa za watoto na akina mama, tumeona ni muhimu kuwa sehemu ya furaha hii kwa kutoa msaada utakaowezesha watoto hawa kupata mahitaji muhimu katika hatua zao za mwanzo za maisha,” alisema Lwiza.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji, hususan watoto na akina mama, kwa kuwa wao ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.





No comments:
Post a Comment