HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 06, 2014

Jaji Mkuu kuzindua Bodi Mpya ya MCT Agosti 7

     Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Agosti 7, mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam.

Bodi hiyo ilichaguliwa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama  wa MCT uliofanyika Juni 25, 2014 mjini Bagamoyo. Rais mpya wa Baraza ni Mhe Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye anachukua nafasi ya Jaji mstaafu, Dr. Robert Kisanga aliyemaliza  muda wake.  Makamu wa rais wa Baraza  ni Bw. Hassan Mittawi ambaye anachukua nafasi ya Bw. Chande Omar Omar ambaye pia amemaliza muda wake. Bwana Mitawi na Bw. Omar ni waandishi nguli wa habari kutoka Zanzibar.

Wajumbe wengine wanaounda Bodi hiyo  ni pamoja na  Bi Rose Haji, Bi  Tuma Abdallah, Bi. Badra Masoud na Bw. Wallace Mauggo ambao wanatoka kwenye tasnia ya habari. Wengine ni Jaji Mstaafu  Juston Mlay, Bw. Ali Mufuruki  na Prof Bernadetha  Killian wanaotoka kwenye  kijamii.

Hii itakuwa ni bodi ya  sita kuchaguliwa tangu kuundwa kwa Baraza la Habari nchini.

 Kabla ya uzinduzi huo, Bodi hiyo mpya itakuwa na kikao chake cha kwanza ambapo pamoja na mambo mengine, itachagua wajumbe wa kamati  mbili za Bodi ambazo ni Kamati ya Fedha na Utawala na Kamati ya Maadili.

Katika uzinduzi huo, MCT  pia itawaaga wajumbe wa Bodi iliyomaliza muda wake iliyoongozwa na Jaji Kisanga. Wajumbe wengine wa Bodi hiyo iliyomaliza muda wake  ni pamoja na Prof.Ruth Meena, Bw. Rafii Haji Makame, Bw. Kenneth Simbaya na Bi. Usu Mallya.

 Kajubi D. Mukaganga
Katibu Mtendaji

No comments:

Post a Comment

Pages