Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiwasalimia maafisa wa Polisi Makamo Makuu ya Polisi Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya Pamoja na Maafisa wa Polisi Ziwani Zanzibar.
Na Hamis Haji, Zanzibar
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim
Seif Sharifa Hamad ametoa wito kwa Jeshi la Polisi Zanzibar kutekeleza majukumu
yao kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha askari hawafanyi kazi kwa
misingi ya upendeleo, chuki, rushwa, wala ubaguzi wa aina yoyote.
Maalim Seif ameyasema hayo leo wakati alipotembelea
Makao Makuu wa Polisi Zanzibar Ziwani, na kuzungumza na Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Hamdan Makame pamoja na maafisa wa Jeshi hilo.
Makamu wa Kwanza amesema kwa kiasi kikubwa Polisi
Zanzibar limepata mafanikio makubwa katika kusimamia majukumu yake, hasa ya kupunguza
matendo ya uhalifu, lakini wapo miongoni mwa askari hujihusisha na matendo yaliyo
kinyume cha maadili yanayolitia doa jeshi hilo.
Alisema zipo taarifa kwamba baadhi ya Maafisa wa
polisi huvujisha taarifa na kuwapa watuhumiwa wa dawa za kulevya, pale jeshi
hilo linapojiandaa kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria.
Maalim Seif amesema tabia hiyo haina budi kukomeshwa
kwa nguvu zote kwa sababu hudhorotesha mikakati ya kukomesha uingizwaji na
biashara ya dawa za kulevya katika visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema dawa za kulevya
zinasababisha madhara makubwa kwa wananchi hasa vijana, na Polisi wanatakiwa
kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti uingizwaji wake kwa kushirikiana na
taasisi za Kitaifa na Kimataifa.
“Nasikia baadhi ya wakati taarifa huvujishwa na
maafisa wa Polisi. Kitengo cha Polizi cha Dawa za Kulevya lazima kiwe na watu
waaminifu sana, Kamishna hili ni tatizo kubwa lazima tulikomeshe”, alisema
Maalim Seif.
Amelipongeza Jeshi hilo kwa juhudi kubwa linazozichukua
kuwakamata watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuwafikisha mbele ya sheria, lakini
hata hivyo amesema bado juhudi zaidi zinahitajika kuwamata wafanyabiashara
wakubwa ambao mara nyingi hawapatikanwi.
No comments:
Post a Comment