HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2014

NOOIJ ATARAJIA MECHI YA WAZI DHIDI YA MSUMBIJI

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema anakiamini kikosi chake ambacho kesho (Agosti 3 mwaka huu) kinacheza mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji (Mambas).

Mechi hiyo ndiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya Tanzania na Msumbiji itakayoingia hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa ajili ya kutafuta tiketi za Fainali itakayofanyika mwakani nchini Morocco.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Timu itakayosonga mbele itaingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia.

Akizungumza hapa Maputo, Nooij amesema anaamini kikosi chake kitacheza vizuri zaidi kuliko kilivyofanya jijini Dar es Salaam kwa vile hakitakuwa katika shinikizo la washabiki ambalo mara nyingi hufanya wachezaji wasijiamini.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia katika hoteli ya Pestana Rovuma ikitokea Johannesburg, Afrika Kusini ambapo ilifanya maandalizi yake mwisho, na itafanya mazoezi leo (Agosti 2 mwaka huu) saa 9 alasiri Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi ya kesho.

Kikosi hicho cha timu ya Taifa leo imeandaliwa chakula cha jioni na Balozi wa Tanzania hapa Msumbiji, Shamim Nyanduga.

Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu nao wameungana na timu leo asubuhi hapa Maputo wakitokea Lubumbashi katika klabu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mechi itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Uganda wakiongozwa na Dennis Batte itaanza saa 9 alasiri kwa saa za hapa ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 10 jioni.

Wachezaji waliopo katika kiosi cha Taifa Stars hapa Maputo ni Aggrey Morris, Aishi Manula, Amri Kiemba, Deogratias Munishi, Erasto Nyoni, Haruna Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Kelvin Yondani, Khamis Mcha, Mbwana Samata, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Oscar Joshua, Ramadhan Singano, Said Moradi, Shabani Nditi, Shomari Kapombe, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
MAPUTO

No comments:

Post a Comment

Pages