HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 31, 2014

BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI LACHOCHEA UBORA WA UTENGENEZAJI SAMANI NCHINI

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Dk Anacleti Kashuliza (wa pili kulia) akiweka saini makubaliano ya ushirikiano kati ya FCDL na TAWOFE katika kuboresha utengenezaji wa samani nchini. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu (wa kwanza kulia) anayeshuhudia makubaliano hayo.
 
Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Furniture Centre (FCDL), na Shirikisho la Watengenezaji Samani Nchini (TAWOFE), wamesaini makubaliano (MoU) kuongeza ubora wa bidhaa za samani zinazotengenezwa nchini na kuzifanya zipate soko ndani na nje ya nchi.

Makubaliano haya yamekamilika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa ni mwendelezo wa Tathimini iliyofanywa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani, katika kuiwezesha sekta ya Samani nchini kupitia vikundi na makampuni ya ndani. 

Tathimini hiyo ya Baraza ya mwaka 2008, ilijikita katika kubaini mahitaji na changamoto zinazoikabili sekta ya samani hapa nchini. 

Baraza liliweza kuandaa warsha iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali na ambapo matokeo ya tathmini hiyo yaliwasilishwa. 

Wadau kutoka sekta ya umma na binafsi walishiriki katika mrejesho wa tathmini hiyo na wao pia kuchangia maoni zaidi kwa ajili ya kuiboresha.

Washirika hao walisaini makubaliano hayo katika  hafla iliyoshuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji wa Uchumi na Uwekezaji), Dk Mary Nagu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dk Anacleti Kashuliza, alisema pamoja na kuwepo kwa fursa kubwa ya soko la samani hapa nchini bado ushiriki wa vikundi na makampuni ya ndani katika soko hilo ni mdogo sana kulinganisha na samani zinazoagizwa kutoka  nje ya nchi.

Alisema tunatoa wito kwa taasisi za Umma na Binafsi  ziunge mkono jitihada hizi kwa kununua samani toka kwa watengenezaji samani  wa ndani na ili kuwapa ushirikiano zaidi utakaowezesha kuimarisha sekta ya samani zitengenezwazo ndani ya nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWOFE, Bw Fredrick Waibi, alielezea makubaliano kati ya FCDL na TAWOFE ni mkakati mzuri utaomjengea uwezo fundi seremala kuweza kutengeneza bidhaa zitakazoweza kukubalika kimataifa, kuongeza tija kazini na kupunguza umaskini kati ya mafundi seremala.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa FCDL, Bw Shafik Bhatia, alisema kama wadau muhimu wa samani nchini wameona umuhimu na wanajivunia  kushirikiana na Tawofe katika kuboresha huduma za samani nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages