HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 27, 2014

MAKALA: "Ni rai yangu, yaliyomkuta Pinda, yasimkute Kikwete"

Na Bryceson Mathias

Mapema 2009 alipokuwa anahitimisha ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako alishuhudia ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alijikwaa Ulimi akasema; “wanaoua Albino nao wauawe”.

Kwa kauli hiyo Pinda alisubiriwa bungeni ajieleze, ambapo Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF) alimbana afafanue kama kauli yake haikuwa inakiuka misingi ya kisheria na haki za binadamu.

Pinda kwa uchungu, alipokosa jibu alibubujikwa machozi, na alipotulia alisema; “Watanzania wataamua kipi kibaya kati ya kauli yake na vitendo vya mauaji ya albino.”

2010, Pinda alipoteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu, tulishuhudia na kusikia mengi, watu walipigwa, wengine kuuawa mikononi mwa polisi, watu wakawa na tafsiri mbalimbali ikiwemo ile ya  “liwalo na liwe” na ..”Piga tuu”….,  ambazo zinadaiwa kuongeza kasi ya mauaji hayo.

Kuibuka kwa tafsiri hizo, kulitokana na swali la nyongeza, la Mbunge wa Kilwa, Murtaza Mangungu, aliyesema,

“Kutokana na hali iliyokuwapo, sasa wananchi wengi wamekuwa na hofu, lakini pia hata shughuli za uzalishaji mali zimeingia kwenye shaka na kuumiza uchumi wa nchi.
 “Serikali ipo tayari kiasi gani kuweza kubainisha na kuchukua hatua stahiki badala ya kusakama makundi fulani. Tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani, ambavyo vyombo vya dola vinashughulikia..??”

“Maana yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, wananchi wanapigwa na vyombo vya dola. Sasa serikali ipo tayari kutoa kauli ni kiasi gani wamefanya uchunguzi na kupata suluhisho la kudumu la matatizo hayo..??” alihoji Mbunge wa Mtwara, Magungu.


Akijibu swali hilo, Pinda alionekana kukerwa na swali la nyongeza, hasa pale mbunge huyo aliposema kuwa wakazi wa Mtwara wanapigwa na vyombo vya dola.

“Hapa unaona anasema (Mangungu) vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo wakati umeambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu, maana hakuna namna nyingine lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria,” alisema na kuongeza:

“Kama wewe umekaidi hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi,  wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu alisema pinda. Kwa sababu hakuna namna nyingine. Maana tumechoka sasa.”

Ya Pinda yasimtokee Kikwete,

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete, alitoa agizo la Ujenzi wa Maabara za Sekondari, ambapo Watendaji nchini wamelifanya zoezi hilo kama Shubiri kwa Wananchi kiasi cha kuwaweka ndani na wengine kutoroka makazi yao na kuishi porini ili kujificha, kwa kushindwa kulipa fedha hizo.

Kibaya zaidi, wananchi wanapohoji mapato na matumizi ya fedha za Maabara ambazo zimechangwa na uhalali wa baadhi ya risiti zinazotumika kuonekana ni Feki, wananchi wanafanyiwa vitendo vya ovyo na watendaji  ikiwemo faini, kupigwa na kuwekwa ndani ndani.

Hapa ndipo ninaposema, kwa vitendo ambavyo wananchi wanafanyiwa na watendaji, vinavyotokana na wao kupata vitisho kutoka kwa  baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya, yaliyompata Pinda,  ni rai yangu; ‘Katu yasimtokea Rais Jakaya Kikwete’.

Tumesikia wananchi wa Kijiji cha Gomba Korogwe, Jumanne Billa, na Ibrahim Ramadhani, wamewekwe ndani kwa kuhoji uhalali wa Risiti za Halmashauri anazotumia, Mtendaji Kata, Boniface Siluli, kukusanyia Michango ya Maabara, huku akikataa ushauri akijiona Mungu Mtu.

Mtendaji huyo alipohojiwa na Mwandishi wa Makala hii alijigamba akisema, 

“Sifanyi kazi za Chadema, wako ninaowafanyia.., Tanzania Daima ni Gazeti la Chadema…” na mimi sifanyi nao kazi”. alipobanwa kwa lugha potofu alibadili., “nafanya kazi ya Wananchi, Kamuulize Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya”.alisema Siluli kwa simu 0713009002.

Mwandishi alimtafuta OCD Madulu wa Korogwe katika simu 0788637679, kama kuna Wanachama Wawili wa Chadema waliowekwa ndani, kwa kosa la kuhoji uhalali wa Risiti Feki za Michango ya Maabara, Magulu alisema hana taarifa hadi afuatilie ofisini kwake.

Mwenyekiti wa Chadema Korogwe, Aulelian Nziku, alikiri Wanachama wake, Billa na Ramadhani, wa Gomba kuwekwa ndani Korogwe, baada ya kuchongewa na Mtendaji Siluli, kwa OCD Magulu na Mkuu wa Wilaya, kwa madai wanazuia Michango, na wakakataliwa dhamana.

Kumekuwa na sintofahamu kwa wananchi, ya kutaka kujua mapato na matumizi ya fedha zilizochangwa kwa ajili ya Maabara, na je risiti zinazotumika za Sh. 10,000/- kwa kila nyumba yenye Mwanamke na Mwanaume na watoto kuanzia miaka 18 ni halali au la? 

“Wananchi tuna hofu kutokana na kutotangaziwa Mapato na Matumizi, ambapo kunatufanya tufikirie fedha zingine zitachotwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.alisema mmoja wao akikataa asitajwe jina akihofu kusurubiwa!

Hata hivyo tumesikia kwenye Vyombo vya Habari, Wananchi wa  Kanda ya Ziwa, Geita, Musoma, nao wamefikia mahali pa kuyakimbia makazi na kwenda milimani kujificha, na kuogopa mkono wa sheria wa watendaji, iwapo watashindwa au kukosa fedha ya kuchangia Maabara.

Kwa upande mwingine, tumemsikia na kumuona kwenye Runinga, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elasto Mbwilo, akiwatisha kuwafukuza kazi watendaji, watakaoshindwa kutimiza malengo ya kujenga Maabara. Je, mtendaji huyo akitishwa hivyo, yeye atamfanyaje mwananchi?.

Mbwilo alitoa vitisho hivyo, baada ya kulalamikiwa kuhusu kwepo kwa baadhi yao kuwekwa ndani, na viongozi wao wa juu, lakini yeye akasema si kuwekwa ndani tu, yeye atawafukuza kazi kazi! Kauli ina hiyo ina maana gani? Si kwamba na wao watumi nguvu kwa wananchi?

Kama mwananchi anashindwa kupata Mulo wa siku moja, atapataje fedha ya kujengea maabara? Kujenga Maabara ni wajibu wa Serikali, isipokuwa wananchi wanatakiwa kushawishiwa na kuwaomba wafanye hivyo kwa ridhaa, badala ya kuwatisha na kuwanyanyasa, ikibidi wasomewa mapato na matumizi wanayotaka kujua.

Iwapo Serikali imeshindwa hata kununua mazao ya wananchi, mfano; Mahaindi, Mpunga na mazao mengine ili wananchi wapate fedha ya kuwakimu na kusaidia maendeleo katika maeneo yao, wananchi watapata wapi fedha kama mazao yao hayanunuliwi?
Serikali ifike mahali ifunguke na kuelewa isifanya hadithi za Alinacha, ni majuzi tu Walimu wamelalamika kuwa wanakatwa fedha kwenye Mishahara yao kwa lazima bila ridhaa, ili kuchangia Ujenzi wa Maabar; Nguvu ya kuwanyanyasa na Walimu na vimishahara vyao vidogo inatoka wapi?

Ni rai yangu watawala waelewe, ‘Wasimuudhi Mchinja Mbwa, Uwazimu Utawarudia
0715933308/0754933308/0786868900

No comments:

Post a Comment

Pages