Na Mwandishi Wetu
MIGOGORO ya kupigania ardhi kati ya Wakulima na
Wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini inatokana na Katiba mbovu iliyopo
sasa.
Kauli hiyo ilitolewa na mmoja wa Wakazi wa Kiteto
mkoani Manyara, Ole Nkoko wakati alipozungumza kwa njia ya simu kuhusu mapigano yanayojitokeza mara kwa mara katika jamii hizo.
“Kama hakutapatikana Katiba inayotambua haki za
wafugaji kama ilivyo kwa Wakulima wote bila ya kubagua wakubwa na wadogo basi
serikali itambue migogoro hii itaendelea hata katika miaka 50 ijayo,”alisema
Ole Nkoko.
Alisema Katiba hiyo inazuia kutengwa kwa maeneo ya
wafugaji na baadala yake wafugaji wamekuwa wakipoteza ardhi na hivyokutishia
uwepo wa ufugaji nchini.
Ole Nkoko, alisema kutokana na mazingira hayo
serikali imekuwa ikiwanyang’anya wafugaji maeneo yao kwa ajili ya utanuzi wa
hifadhi ya wanyama pori, kilimo cha mashamba makubwa, utanuzi wa miundo mbinu
ya majeshi ya ulinzi na usalama.
“Pia kuna visingizio vingi vinavyotolewa na baadhi
ya viongozi kuwa wafugaji wanaharibu mazingira, hili halina ukweli,”alisema Ole Nkoko.
Ole Nkoko, alisema kama wananchi watakumbuka,
serikali iliwahi kutenga maeneo maalum ya mashamba kwa ajili ya mazao kama
pamba, kahawa, tumbaku na katani lakini cha kushangaza haijawahi kutenga maeneo kama hayo kwa ajil
ya mifugo hali ambayo inachangia
wafugaji hao wanaponyang’anywa maeneo yao kusambaa wakitafuta malisho.
“Tumetenga
hata maeneo malum kwa ajil ya pundamila (hifadhi za taifa), lakini wafugaji
wananing’inia hewani tu,”alisema hiyo ni kauli ya Mwalimu Nyerere, aliyoitoa Morogoro,
mwaka 1981.
Ole Nkoko alisema sasa wafugaji wamekuwa kama watoto
yatima wakihangaika huku na kule kwa ajili yakutafuta malisho ya mifugo yao
ambapo wakati mwingine huzusha migogoro na wakulima.
Akizungumzia mgogoro wa Kiteto, Ole Nkoko, alisema
mgogoro huo unaonekana ufumbuzi wake uko mbali kutokna na viongozi kutoonesha
utashi wa kuumaliza na kuendelea kwake huenda ukawa na maslahi binafsi ya
viongozi hao kisiasa.
Alisema kwa mfano mwaka huu viongozi mbalimbali
akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu wa chama
cha mapinduzi CCM Abrahamani Kinana walitembelea eneo hilo huku wakishindwa
kuupatia ufumbuzi zaidi ya kutoa ahadi ya kutafuta suluhu bila mafanikio.
Inadaiwa
tangu kuibuka mgogoro huo Januari mwaka huu zaidi ya watu 30 wameuawa na
wengine 200 kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment