WASAFIRISHAJI abiria kwa kutumia bajaji na bodaboda jijini
Dar es Salaam, wamelaani kitendo cha serikali cha kuwakamata wanapoingia katika
ya jiji kwa madai kuwa ni kinyume cha sheria.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam wasafirishaji hao, walisema kinachofanywa na serikali ni uonevu kwa sababu
watu hao wanajitafutia riziki kwa ajili ya familia zao.
Mmoja wa Wasafirishaji hao, Mohamed Juma ambaye ni mmoja
kati ya watu wenye ulemavu, alisema wanaalani kitendo hicho kwa sababu serikali
yenyewe ndio imeamua kuingiza vyombo hivyo ili kupunguza tatizo la ajira kwa
vijana, ambalo ni sawa na bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.
Alisema, wanashangaa kuona serikali ikiwashupalia wakafanye
biashara hiyo pembezoni mwa jiji wakati wakijua fika kwamba hata huko nako yapo
makundi ya vijana wanaofanya biashara hiyo.
“Unajua hii biashara ya usafirishaji inafanywa na makundi ya
vijana katika maeneo mbalimbali ya jiji hivyo siyo rahisi kwa kutuondoa sisi
tulioko katikati ya jiji na kutupeleka kwingine ambako nako tayari wapo, hii inaweza
ikazusha ugomvi wa kimaslahi,”alisema Juma.
Juma, alisema watajaribu kutafuta muafaka na serikali kuhusu
suala hilo na endapo itashindikana huenda huko mbeleni wakafikiria kurudisha
vyombo hivyo serikalini kwa pamoja.
Charles James, muendesha bodaboda alisema, kama biashara
hiyo ni haramu kufanyika katikati ya jiji basi ni vema serikali ikasimamisha uingizaji
wa vyombo hivyo ambavyo vinadaiwa kuingizwa kwa wingi bandarini kuliko mzigo
wowote.
“Sio kweli kama wamesimamisha operesheni hiyo kama
wanavyodai baadhi watu eti kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,”alisema James.
James, alisema hata kama ikitokea hivyo hadhani kama kuna
ulazima wa kushangilia, kwa sababu bado tatizo lipo la kuvunjwa haki zao ambazo
ni kuuziwa vyombo hivyo kisha kuwekewa mipaka ya matumizi.
Alisema wakati watu wenye ulemavu wakijiaandaa kuvikusanya
vyombo hivyo na kwenda kuvirundika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadik,
wao waendesha bodaboda wanajipanga jinsi ya kujiunga nao katika kadhia, hata
hivyo hawakufafanua lini watafanya
hivyo.
No comments:
Post a Comment