Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na
bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi
chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Algeria kuwania kufuzu
kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari leo, Mkwasa amesema
wamejiandaa kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo, wanajua
Algeria ni miongoni mwa timu bora Afrika, lakini hilo halitawazuia
kuibuka na ushindi.
“Katika mpira wa sasa duniani hakuna timu kubwa wala timu ndogo,
lolote linaweza kutokea, sisi tuna nafasi ya kufanya vizuri tukiwa
katika uwanja wa nyumbani na washabiki wetu” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa alisema wamefanya mazoezi kwa pamoja kwa takribani siku
10, vijana wapo katika hali nzuri, hakuna majeruhi vijana wote wapo
katia hali nzuri na timu imefanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi kabla ya
kushuka dimbani kuwakabili Mbweha wa Jangwani.
Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa
Taifa kuja kuwapa sapoti vijana watakapokuwa wanapeperusha bendera ya
Tanzania.
No comments:
Post a Comment